KATIBU Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dkt. John Jingu,akizungumza wakati akifungua kikao cha Makatibu Wakuu na Manaibu Makatibu Wakuu kuhusu Mafunzo ya Usawa wa Kijinsia na Tathimini ya Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) kilichofanyika Jijini Dodoma.
KATIBU Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Zainab Chaula,akizungumza wakati wa kikao cha Makatibu Wakuu na Manaibu Makatibu Wakuu kuhusu Mafunzo ya Usawa wa Kijinsia na Tathimini ya Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) kilichofanyika Jijini Dodoma.
SEHEMU ya Washiriki wakifatilia mada mbalimbali wakati wa kikao cha Makatibu Wakuu na Manaibu Makatibu Wakuu kuhusu Mafunzo ya Usawa wa Kijinsia na Tathimini ya Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) kilichofanyika Jijini Dodoma.
……………………
Na Alex Sonna-DODOMA
KATIBU Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dkt. John Jingu ameitaka jamii, wadau na kila mmoja kwa nafasi yake kukemea vitendo vya ukatili dhida ya Wanawake na Watoto ambavyo vimekuwa vikiripotiwa katika maeneo mbalimbali nchini.
Hayo ameyasema hayo Jijini Dodoma kwa niaba ya Katibu Mkuu Kiongozi wakati akifungua kikao cha Makatibu Wakuu na Manaibu Makatibu Wakuu kuhusu mafunzo ya Usawa wa Kijinsia na Tathimini ya Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA).
Dk.Jingu amesema licha ya mafanikio yaliyopo kufuatia juhudi zinazofanywa kukabiliana na vitendo hivyo lakini bado ukatili umeendelea kufanywa hivyo ipo haja ya kuwa na afua mbalimbali za kuwatetea manusura wa vitendo hivyo.
“MTAKUWWA lengo lake ni kutokomeza ukatili wa aina zote unaofanywa katika jamii zetu sasa ukatili bado upo hivyo tumekubaliana kila mmoja wetu awe kinara wa mabadiliko chanya kuhakikisha tunakuwa na malezi bora, afua za kuyalinda makundi yote,”amesema Dkt. Jingu.
Hata hivyo ametoa wito kila kundi kwa nafasi yake Wizara za Kisekta, Taasisi za Serikali, Mashirika ya Kimataifa, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, Viongozi wa Dini, Wazee wa Kimila na Vyombo vya Habari yana sehemu ya kufanya kwa kuongeza juhudi za kuimarisha usawa wa jinsia na kutokomeza ukatili .
“Nitoe rai tuendelee kushirikiana ili tuweze kutokomeza vitendo vya ukatili katika jamii na kufikia malengo na mikakati tuliyojiwekea na nishukuru wadau wote kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali na kuhakikisha makundi yote yanalindwa dhidi ya ukatili wa kijinsia ,”amefafanua Dkt. Jingu.
Amesema kuwa miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa ni pamoja na kuwepo kwa Mpango maalumu wa malezi ya vijana balehe ili waweze kukua katika maadili, kujitambua na kufahamu nafasi yao kwa jamii.
Dkt. Jingu ameeleza kuwa uzingatiaji wa bajeti kwa mtizamo wa kijinsia katika Sera, Mipango na Bajeti za Wizara na Sekta utasaidia kuleta maendeleo endelevu katika nyanja zote za Kijamii.
“Uandaaji wa bajeti na mipango kwa mtizamo wa kijinsia una manufaa makubwa sana katika jamii yetu kama kushughulikia upungufu wa kijinsia hususan ule unaotokana na uwepo wa mahitaji tofauti baina ya wanawake na wanaume katika jamii au sehemu zetu za kazi,” Amesema.
Aidha amewashukuru Wadau wa Maendeleo, Taasisi za serikali na binafsi, viongozi wa dini, kimila na mtu mmoja mmoja kwa kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuimarisha usawa wa jinsia na kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto hapa nchini.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Zainab Chaula amewataka maafisa maendeleo kupitia ngazi ya Vijiji, Kata hadi Wilaya kutimiza wajibu wao kuhakikisha maendeleo yanapatikana, wananchi wanakuza uchumi wao na kushiriki katika maendeleo kwa kulipa kodi.
“Kupitia mafunzo haya tumeongea mambo mengi yakiwemo mpango wa Kitaifa wa malezi kwa makundi ya vijana balehe ambao una malengo mengi kama kuzuia UKIMWI, mimba za utotoni, ajira na matumizi ya dawa za kulevya pamoja na kumuandaa mtoto kuwa kiongozi bora kuanzia ndani ya familia,”amesema Dkt. Chaula
Awali Mratibu wa Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokemeza Ukatili dhidu ya wanawake na Watoto kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Bw. Joel Mangi,amesema kuwa tangu kuanza kwa mpango huo mwaka 2017/18 na 2021/2022 ambao umekamilika na kufanyika kwa tathmini ambayo imefanikiwa kwa kiasi kikubwa ikiwemo kuongezeka kwa uelewa ndani ya jamii, uanzishwaji wa vituo 21 vya huduma kwa manusura wa ukatili ambapo vinafanya kazi nchi nzima.
“Mwelekeo katika awamu ijayo tumependekeza kuanzishwa kwa kampeni jumuishi ya Kitaifa itakayoleta sekta zote pamoja kupaza sauti , tuimbe kupinga ukatili huu jamii ijue vitendo hivi havifai kwa sababau vinazorotesha ustawi hasa kwa watoto ,”amesema Mangi