Waziri wa Maji, Prof. Makame Mbarawa akimsikiliza Kaimu Meneja RUWASA Wilaya ya Ruangwa, Mhandisi Lawrence Mapunda anayetoa maelekezo kuhusu Mradi wa Maji wa Mihewe unaotumia teknolojia ya kuchuja chumvi kwenye maji (Reverse Osmosis), mkoani Lindi.
Mashine inayotumia teknolojia ya kuchuja chumvi kwenye maji (Reverse Osmosis) inayotumika kwenye Mradi wa Maji wa Mihewe katika Wilaya ya Ruangwa, mkoani Lindi.
Waziri wa Maji, Prof. Makame Mbarawa akitoa maelekezo ya kumsimamisha Mkandarasi wa Kampuni ya Syscon Builders Ltd (katikati) anayetekeleza Mradi wa Maji wa Narungombe katika Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi, baada ya kushindwa kumaliza mradi licha ya kuongezewa muda wa miezi miwili.
Mafundi wakiwa eneo la ujenzi wakiendelea na kazi ya ujenzi wa tenki la maji la Mradi wa Maji wa Kitandi katika Wilaya ya Ruangwa, mkoani Lindi.
Waziri wa Maji, Prof. Makame Mbarawa akitoa maelekezo mara baada ya kukagua chanzo cha maji cha Ruponda kinachotumika na Mradi wa Maji wa Mandawa katika Wilaya ya Nachingwea, mkoani Lindi.
Wananchi katika Kijiji cha Nammanga wakifurahi na Waziri wa Maji, Prof. Makame Mbarawa pamoja na Mbunge wa Jimbo la Nachingwea, mkoani Lindi Hassan Masala baada ya Waziri wa Maji kutoa ahadi kiasi cha Shilingi milioni 246 ili kumaliza tatizo la maji katika kijiji hicho.
…………………..
Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa ameelekeza Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa ichukue hatua haraka za kisheria za kuvunja mkataba na Mkandarasi wa Kampuni ya Syscon Builders Ltd mwenye kazi ya ujenzi wa Mradi wa Maji wa Narungombe wenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 310 baada ya kukuta mradi huo umekwama kwa sababu ya kukiuka masharti ya mkataba.
Maamuzi ya Prof. Mbarawa yamekuja baada ya mkandarasi huyo kukiri kulipwa fedha zaidi ya Shilingi milioni 105 sawa na asilimia 33 ya jumla ya fedha zilizopangwa kutekeleza mradi na kuzitumia kwa matumizi mengine nje ya makubaliano ya mkataba.
Profesa Mbarawa amesema mkandarasi huyo alitakiwa awe amekamilisha mradi huo tangu mwezi Februari, 2018 na licha ya kuomba muda wa nyongeza wa miezi miwili, mradi haujakamilika na bado anaomba muda mwingine wa nyongeza, wakati wananchi wa Kijiji cha Narungombe wakiendelea kuwa na tatizo la maji.
‘‘Kimsingi mkandarasi huyu hawezi kumaliza mradi huu hata tumpe mwaka mzima, ni mbabaishaji na hata wananchi hawana tena imani nae kwa kuwa ameshatoa ahadi ya uongo kukamilisha mradi huu’’, amesema Prof. Mbarawa.
‘‘Nikuombe Mwenyekiti na viongozi wa Halmashauri mfuate taratibu za kisheria mvunje mkataba na huyu mkandarasi na kazi hii ifanywe na Mamlaka ya Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) ndani ya muda mfupi iwe imekamilika tumalize kero ya maji Narungombe’’, ameelekeza Waziri Mbarawa.
Mradi wa Maji wa Narungombe ni miongoni mwa miradi ya maji minne ambayo ilikuwa inatekelezwa na Halmashauri ya Ruangwa kupitia fedha za Serikali Kuu kwa kusanifiwa na kusimamiwa na wataalam wa Halmashauri wenyewe. Ambapo ujenzi wake ulianza mwezi Septemba, 2018 na ulitarajiwa kukamilika mwezi Septemba, 2019.
Aidha, Prof. Mbarawa amesema Serikali itatoa fedha za matengenezo ya mashine ya Mradi wa Maji wa Mihewe katika Wilaya ya Ruangwa unaotumia teknolojia ya kuchuja maji yenye chumvi (Reverse Osmosis) baada ya kuharibika kwa vichujio (membranes) na kusababisha adha ya maji kwa wananchi. Pia, itabadilisha mfumo wa uendeshaji wa mradi huo kutoka kwenye matumizi ya jenereta na kuanza kutumia nishati ya jua ili kupunguza gharama kubwa za matumizi ya mafuta.
Akizungumza na Waziri wa Maji, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Ruangwa, Rashid Nakumbya amesema mradi huo ni muhimu kwa halmashauri hiyo ukizingatia kuwa wanatarajia kuanza kwa mradi wa uchimbaji wa madini ya bunyu (graphite). Vilevile, wanategemea ongezeko kubwa la watu na kufanya huduma ya uhakika ya maji kuwa ni lazima.
Katika hatua nyingine, Waziri wa Maji, Prof. Mbarawa amesema atatuma kiasi cha Shilingi milioni 246 mwezi Oktoba, 2019 kwa Halmashauri ya Nachingwea kwa lengo la kumaliza tatizo la maji kwenye Kijiji cha Nammanga kwa kufanikisha ujenzi wa mradi wa maji, jambo lililopokewa kwa shukrani na furaha kubwa na wananchi hao.
Prof. Mbarawa amekagua miradi ya maji ya Mihewe, Narungombe na Kitandi katika Wilaya ya Ruangwa, Mradi wa Maji wa Mandawa pamoja na kuzungumza na wananchi wa vijiji vya Nammanga, Mandawa na Namikango katika Wilaya ya Nachingwea.