Balozi wa Tanzania nchini Msumbiji Mheshimiwa Humphrey Polepole alipofanya ziara ya kutembelea  eneo la bandari Ndumbi wilayani Nyasa mkoani Ruvuma ikiwa ni ziara ya kuangalia fursa za uwekezaji katika ushoroba wa Mtwara unaonzia bandari ya Mtwara hadi bandari ya Mbambabay 

Balozi wa Tanzania nchini Malawi Mheshimiwa Humphrey Polepole akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma katika eneo la bandari kongwe ya Mbambabay wilayani Nyasa

**********************

SERIKALI inatarajia kuanzisha Kanda Maalum ya kiuchumi {Special Economic Zone}  katika eneo  la Mbambabay ziwa Nyasa  Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma ili kuhakikisha bidhaa zote ambazo zinapatikana Kariakoo jijini Dar es salaam ziweze kupatikana Nyasa.

Hayo yamesema na Balozi wa Tanzania nchini Malawi Mheshimiwa Humphrey Polepole alipofanya ziara ya siku moja  mkoani Ruvuma katika wilaya ya Nyasa kuangalia fursa za uwekezaji katika ushoroba wa Mtwara,unaonzia mkoani Mtwara hadi Mbambabay ziwa Nyasa.

Akizungumza baada ya kukagua bandari Kongwe ya Mbambabay na bandari mpya ya Ndumbi ambayo serikali imetoa zaidi ya shilingi bilioni 12 kujenga bandari hiyo,Balozi Polepole  ametoa rai kwa wadau kuwa tayari kutumia fursa zote zinazopatikana katika ushoroba wa Mtwara.

“Ushoroba huu ni wa barabara inayotoka bandari ya Mtwara na inakuja kwa kilometa 822 mpaka bandari ya Mbambabay,ushoroba huu katika kusini mwa Afrika,ndiyo ushoroba bora zaidi na  mfupi kuliko shoroba nyingine zote’’,alisema.

Amesema ushoroba wa Mtwara umesheheni madini ya aina mbalimbali yakiwemo makaa ya m awe,dhahabu,uranium na madini mengine ambayo ni fursa kwa wakazi wa eneo lote la ushoroba.

Polepole amesema wamedhamiria kuhakikisha ushoroba wa Mtwara unatangazwa na kuwa mbadala wa ushoraba wa Dar es salaam kwa sababu Dar es salaam hadi Lilongwe ni Kilometa 1600 wakati Ushoroba wa Mtwara ni kilometa 900.

Balozi huyo wa Tanzania nchini Malawi amesema kutokana na hali hiyo ametoa rai kwa Mamlaka ya Bandari Tanzania TBA kuboresha miundombinu ya bandari ziwa Nyasa ili serikali ivune pesa na  kukusanya kodi kwenye ushoroba huu kutoka nchi za Malawi,Msumbiji,Zambia na Zimbabwe.

Amesema serikali ina mipango mikubwa ya kuwezesha usafirishaji wa shehena ya mizigo zaidi ya tani laki moja  ambayo itawezesha milango ya kibiashara kufunguka katika bandari za Mtwara,Mbambabay,na ushoroba wote wa Mtwara.

Ametoa katika nchi ya Malawi tayari ubalozi umepokea maombi ya wafanyabiashara ambao wapo tayari  kujiridhisha utayari wa ushoroba wa Mtwara ili waanze kupitisha shehena za mizigo kupitia ushoroba wa Mtwara.

”Sisi kama ubalozi wa Malawi,tumetoa ombi maalum kwa Mkoa wa Ruvuma hususan wilaya ya Nyasa,kuhakikisha  tunaanzisha eneo maalum la kiuchumi ambalo linawezesha kupatikana  bidhaa zote ambazo zinapatikana Kariakoo jijini Dar es salaam ziweze kupatikana Mbambabay’’,alisisitiza.

Amesema ili kuhakikisha suala hilo linafanikiwa kwa asilimia 100,meli ya abiria ya Mbeya II katika ziwa Nyasa hivi karibuni inatarajia kuanza safari za kuvuka ziwa kutoka Bandari ya  Mbambabay Tanzania na Kwenda nchini Malawi katika bandari za Ntakabay,Chilumba na Chipoka ambako watafarishwa wafanyabiashara na mizigo kuja Mbambabay na kununua bidhaa mbalimbali zitakazokuwepo  baada ya kuwa kituo cha kiuchumi.

Amesema bidhaa hizo zitakwenda nchini Malawi hadi Bandari ya Tete nchini Msumbiji kupitia ziwa Nyasa ambayo itakuwa ni  fursa kubwa ya kibiashara  wa Tanzania nan chi jirani.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas  akizungumzia uwekezaji uliofanyika katika bandari ya  Ndumbi,amesema serikali imewekeza mabilioni ya fedha kutekeleza mradi huo ambao umekamilika.

Amesema Mkoa umejiandaa kuanzisha maeneo maalum kwa ajili ya uwekezaji ambapo hivi sasa bidhaa zote ambazo zitahitajika katika nchi Jirani  zitapatikana katika bandari ya Mbambabay ziwa Nyasa ili kupunguza umbali wa Kwenda Dar es salaam.

Ametoa rai kwa wafanyabiashara wa Tanzania kuchangamkia fursa hiyo na kwamba serikali ipo tayari kuwawezesha miundombinu yote inayohitajika ili bidhaa zote ziweze kupatikana katika wilaya ya Nyasa.

 Naye Mkuu wa Wilaya ya Mbinga ambaye pia ni Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Mheshimiwa Aziza Mangasongo amesema kukamilika kwa mradi wa bandari ya Ndumbi kunafungua fursa mpya za uwekezaji mkoani Ruvuma.

Imeandikwa na Albano Midelo

Afisa Habari Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ruvuma

Septemba 8,2022