**************************************
Na Ahmed Mahmoud Arusha
Chama cha mawakala wa forodha( TAFFA) Mpakani Namanga,wilayani Longido, wamemwomba Waziri mkuu, Kassimu Majaliwa kuingilia kati mgogoro kati yao na wakala wa vipimo (WMA) unaowalazimisha kulipia tozo mpya inayotozwa kwa kila bidhaa badala ya kutumia utaratibu wa awali wa kulipia tozo kwa mzigo wote.
Aidha wamesema hawapo tayari kufanya kazi na wakala hao hadi hapo watakapo onyeshwa hiyo sheria mpya ambayo wanalazimishwa kuitekeleza bila kuwepo kwa mwongozo wowote kutoka serikalini kitendo ambacho kinawaumiza zaidi.
Msimamo huo waliutoa Jana kwenye mkutano wao uliokuwa ukiongozwa na mwenyekiti wao, Ismail Kilas uliofanyika eneo hilo la Namanga, wilayani Longido,Mkoani hapa.
Mawakala hao walisema kuwa, walikuwa wakitumia sheria ya zamani ya mwaka 2016 ambayo walikuwa wakilipia asilimia 0.2 ya thamani ya mzigo ambapo kiwango cha chini cha malipo ilikuwa ni sh, 100,000 kwa mzigo.
Walisema wanachopinga ni wakala wa vipimo kuamua kuwatoza malipo ya shilingi laki moja kwa kila aina ya bidhaa (item ) badala ya mzigo mzima Kama sheria inavyoelekeza .
“Tunamwomba waziri mkuu aje Namanga kuja kuzungumza na sisi juu ya huu mgogoro Kwani tukiendelea na utaratibu huu tutakosa wafanyabiashara kwani hakuna mtu aliye tayari kupata hasara kwani jinsi tunavyopandishiwa gharama za tozo ndivyo hivyo hivyo bei za bidhaa zitakavyopanda .”alisema Kilas
Naye Meneja wa tawi wa kampuni ya EDPAC ,Wilson Kazen alisema kuwa, kwa sasa hivi hawapo tayari tena kufanya shughuli yoyote bila kupata muongozo wa sheria mpya inayowalazimu wao kutumia utaratibu mpya wa kulipa tozo ya laki moja kwa kila bidhaa badala ya mzigo Kama utaratibu wa awali.
Alisema kuwa, walipokea barua mnamo may 15 mwaka huu ya ufafanuzi wa kanuni ya ada za ukaguzi wa bidhaa zilizofungashwa zinazoingia nchini kutoka nje ya nchi kutoka kwa kaimu meneja wa wakala wa vipimo mkoa, Dismas Maturine inayohusu wao kulipia bidhaa moja moja badala ya kutozwa kwa mzigo mzima kama ilivyokuwa hapo awali bila kushirikishwa chochote kabla ya kupewa barua hiyo.
Naye Janeth Mero kutoka kampuni ya Beam Tanzania Ltd alisema kuwa, uwepo wa utaratibu huo wa kulipa kwa kwa mzigo mmoja mmoja unatengeneza mazingira ya rushwa, hivyo kuwataka kuendelea kwa ule utaratibu uliokuwepo wa awali ili waendelee kulipa bila migogoro yoyote.
“Ni wiki moja sasa magari yamesimama kusafirisha mizigo kutokana na mgogoro uliopo na Wakala wa vipimo tunachotaka waziri Mkuu Majaliwa aje atusikilize” AlisemaJaneth
Kwa upande wake mkurugenzi wa ufundi kutoka wakala wa vipimo makao makuu, Stella Kahwa alisema kuwa, amesikiliza malalamiko hayo na yamepokelewa na yanaendelea kufanyiwa kazi na kusema kuwa, utaratibu utakaoendelea kutumika ni ule uliokuwa ukitumika awali wa kulipia laki moja kwa mzigo.
“Nikweli tumepata malalamiko ya Mawakala wa Forodha tumeyapokea na yanaendelea kufanyiwa kazi na tumeamuru waendelee na utaratibu wao wa kawaida kwa kufuata kanuni ya mwaka 2016 ya mwongozo wa sheria” Alisema Stella.