Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan anaondoka nchini leo kuelekea Accra, Ghana kwa ajili ya Ziara ya Kikazi ya siku tatu nchini humo.
Akiwa nchini Ghana, Mhe. Rais Samia anatarajia kushiriki Mdahalo wa Wakuu wa Nchi utakaojadili fursa zilizomo na changamoto zinazozikabili Nchi za Afrika ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa athari za mabadiliko ya tabianchi, kupanda kwa bei ya vyakula na matumizi ya nishati endelevu.
Mhe. Rais Samia pia anatarajia kupokea Tuzo ya mwaka 2022 ya Babacar Ndiaye kwa mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita katika ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji ambayo hutolewa kwa Mkuu wa Nchi iliyofanya vizuri zaidi.
Tuzo hiyo hutolewa kila mwaka katika Mkutano wa AfDB, ambao kwa mwaka 2022 unafanyika Accra, Ghana.