Mkurugenzi mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania(TAEC) Profesa Lazaro Busagala(katika chini) katika picha ya pamoja na washiriki 30 kutoka nchi 21 kwenye ufunguzi wa mkutano wa uboreshani wa Usalama wa Uhifadhi wa mabaki ya vyanzo vya Mionzi unaofanyika jijini Arusha
…………………
Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) kwa kushirikiana na Shirika la Nguvu za Atomiki Duniani (IAEA) inafanya mkutano wa kimataifa kwa ajili ya kuboresha usalama katika kuhifadhi mabaki ya vyanzo vya mionzi
Mkutano huu wa siku tano umewakutanisha watalaamu 30 kutoka katika nchi 21 duniani unaendelea jijini Arusha. Lengo kuu la mkutano huu ni kujadili kwa pamoja mkakati wa kuboresha usalama wakati wa kuhifadhi mabaki ya vyanzo vya mionzi ili kuepusha madhara ya vyanzo vya mionzi kwa binadamu na mazingira.
Mkurugenzi Mkuu wa TAEC Prof. Lazaro Busagala amesema jukumu la kusimamia usalama wa vyanzo vya mionzi sio la taifa moja, bali linahitaji ushirikiano wa nchi zote Duniani ili kuhakisha kwamba vyanzo vyote vya mionzi vinakuwa katika mikono salama ili kuepusha madhara mbalimbali ikiwemo kutumika kwa vyanzo hivyo katika masuala ya ugaidi.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Shirika la Nguvu za Atomiki Duniani (IAEA) Dkt David Bennet amesema kwamba IAEA itaendelea kushirikiana na nchi wanachama ili kuhakikisha kuwa teknolojia ya nyuklia inatumika kwa matumizi salama.
Vyanzo vya mionzi vinapomaliza muda wake wa matumizi vinahitaji kuhifadhiwa mahali salama na palipo na ulinzi maalumu jambo ambalo inasaidia kuepusha vyanzo hivyo kuzagaa na kusababisha madhara mbalimbali kwa binadamu na mazingira.