Afisa Usalama wa chakula wa shirika la viwango Tanzani ( TBS) Aberl Deule ,akizungumza na wandishi wa habari mara baada ya kuteketeza bidhaa za chakula na vipodozi visivyokuwa na ubora zenye thamani ya Sh. Milioni 26.4 katika eneo la taka chidaya jijini Dodoma.
Baadhi ya bidhaa za chakula na vipodozi visivyokuwa na ubora zenye thamani ya Sh. Milioni 26.4 zilizoteketezwa na Shirika la viwango Tanzani ( TBS) katika eneo la taka chidaya jijini Dodoma.
Trekta likiteketeza bidhaa za chakula na vipodozi visivyokuwa na ubora zenye thamani ya Sh. Milioni 26.4 katika eneo la taka chidaya jijini Dodoma.
……………………………………………………………….
Na.Alex Sonna,Dodoma
SHIRIKA la viwango Tanzania (TBS) kanda ya kati limeteketeza bidhaa za chakula na vipodozi visivyokuwa na ubora zenye thamani ya Sh. Milioni 26.4.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma wakati wa uteketezaji wa bidhaa hizo Mkaguzi TBS kanda ya kati Domisiano Rutahala, amesema kuwa zimepatikana kwenye maeneo mbalimbali ya biashara.
Rutahala amesema maeneo hayo ni maduka na migahawa, baa, hoteli na stoo zilizopatikana katika halmashauri zote za mikoa ya Dodoma, Singida na Tabora ambazo zinaunda kanda ya kati.
Aidha amesema bidhaa zilizoteketezwa zimetokana na kaguzi zilizofanyika kwenye maeneo tajwa kati ya Januari hadi Oktoba, 2021.
“Jumla ya kilo 4,056,596 zenye thamani ya Sh. 26,448,500 zimeteketezwa, ikijumuisha bidhaa za chakula na vipodozi zilizoisha muda wa matumizi, zenye viambato sumu na zile ambazo tarehe za mwisho wa matumizi zimehaririwa”amesema
Aidha, amesema uwapo wa bidhaa zilizoisha muda wa matumizi na zile zenye viambato sumu zinaathiri uchumi wa nchi pamoja na afya za watumiaji.
Pia amefafanua kuwa bidhaa za chakula zilizoisha muda wa matumizi na zile ambazo tarehe za mwisho wa matumizi zimehaririwa zinaathiri upatikanaji wa virutubisho vinavyotegemewa, zinaweza kusababisha magonjwa ya muda mfupi na mrefu ikiwemo saratani.
“Kwa upande wa vipodozi hasa vile vyenye viambato sumu athari zake ni za muda mfupi ikiwemo kuathiri ngozi ,macho,mfumo wa uzazi kwa akina mama, ukuaji kwa watoto na magonjwa ya saratani hasa ngozi”alisema
Hata hivyo, amesema kuwa kaguzi hizo ni endelevu kwa mikoa yote, na kutoa wito kwa wafanyabiasahra kukagua bidhaa zao mara kwa mara kujiridhisha na ubora wake.
“Kutunza bidhaa hizo kwa mujibu wa taratibu za wazalishaji, kuepuka kuuza bidhaa za vipodozi zenye viambato sumu na kuacha mara moja kuhariri taarifa za mwisho wa matumizi”amesema
Hata hivyo, alisema kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa wafanyabiashara wasio waaminifu kwa mujibu wa sheria na kanuni zake.