WAZIRI wa Elimu Sayasi na Teknolojia Prof.Joyce Ndalichako,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Oktoba 23,2021 jijini Dodoma wakati akitoa taarifa kuhusu utekelezaji wa mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Tsifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19.
Waandishi wa habari pamoja na watendaji wa wizara wakifatilia hotuba ya Waziri wa Elimu Sayasi na Teknolojia Prof.Joyce Ndalichako,wakati akitoa taarifa kuhusu utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19 leo Oktoba 23,2021 jijini Dodoma.
……………………………………………….
Na.Alex Sonna,Dodoma
SERIKALI kupitia wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia imetoa maelekezo kwa watendaji wa wizara pamoja na taasisi zitakazotekeleza miradi wahakikishe maandalizi ya mpango wa matumizi ya fedha zilizotolewa na Shirika la fedha la kimataifa (IMF) yanakamilika ndani ya Octoba 30 mwaka huu sambamba na kutoa mpango wa utekelezaji wa miradi itakavyofanyika.
Hayo yamesemwa leo Octoba 23,2021 jijini Dodoma na Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako wakati akitoa taarifa huhusu utekelezaji wa mpango wa maendeleo kwa ustawi wa taifa na mapambano dhidi ya uviko 19, ambapo amewataka watendaji wa wizara na taasisi zilipo chini yake kuhakikisha mpango wa utekelezaji wa miradi unatolewa haraka.
Waziri Ndalichako amesema kuwa sekta ya Elimu imetengewa bilioni 368.9 na Wizara ya Elimu imepata shilingi bilioni 64.9 kutekeleza miradi iliyochini ya Wizara hiyo.
Amesema kuwa hadi ifikapo Octoba 30, 2021 kila taasisi itakayotekeleza mradi huo iwe imekamilisha maandalizi na mipango ya utekelezaji pamoja na kuandaa mpango kazi utakao ainisha hatua mbalimbali za taratibu za manunuzi ya huduma na vifaa.
“Hadi tarehe 30 mwezi huu kila taasisi iwe imekamilisha na iainishe lini vifaa vitanunuliwa, vifaa vyote vinunuliwe kwa kuzingatia bei ya soko nataka na mimi nikienda kununua kifaa bei iwe ndio hiyo” amesema Prof. Ndalichako.
Hata hivyo ameagiza miradi hiyo kuhakikisha inakamilika kabla au ifikapo May 30, 2022 na kusisitiza matokeo ya utekelezaji wa mradi yaendane na thamani ya fedha zilizotolewa na si vinginevyo.
“Namuagiza Katibu Mkuu wa Wizara aandae mfumo wa uratibu, usimamizi na ufuatiliaji wa miradi utakaowezesha kubaini changamoto zitakazo kuwa zikijitokeza na kuchukua hatua stahiki na kwa wakati” amesisitiza.
Katika hatua nyingine Waziri Ndalichako amewatahadharisha kuwa fedha hizo hazihusishi ulipanaji wa posho ya aina yoyote na viongozi wa taasisi zinazohusika na kwamba yeye atafuatilia kwa ukaribu katika utekelezaji wa miradi hiyo.
‘Nitafuatilia kwa karibu kuhakikisha maagizo ya Mheshimiwa Rais kuhusu matumizi sahihi ya fedha hizo yanatekelezwa kikamilifu.
”Nawapa tahadhari watumishi wote wa Wizara wanaohusika na utekelezaji wa Mpango huu kuwa nitakuwa makini katika kuhakikisha kuwa mpango huu unatekelezwa kwa ufanisi kuanzia hatua ya maandalizi hadi utakapokamilika kwa wakati uliopangwa.”amesema
Pia Waziri Ndalichako amebainisha kuwa fedha hizo zitakwenda kuimarisha ufundishaji kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu ambapo shilingi bilioni 1.47 zimetengwa, kuimarisha elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi ambapo kiasi cha shilingi bilioni 57.98 zimetengwa na kuimarisha mazingira ya utoaji elimu ya ualimu ambapo kiasi cha shilingi bilioni 5.44 zimetengwa.