Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akifungua kikao kinachohusu tathmini ya utekelezaji wa mpango wa jamii shirikishi na harakishi wa utoaji wa chanjo ya UVIKO 19 kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea.Kushoto kwake ni Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Dr.Jairy Kanga,kikoa hicho kilishiriisha wadau mbalimbali toka mkoani Ruvuma ambacho pia kilitumika kutambulisho chanjo ya pili aina ya sinopharm ambapo Mkoa wa Ruvuma umepata dozi zaidi ya 31,000
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Dr.Jairy Kanga akizungumzia chanjo ya pili ya UVIKO 19 aina ya sinopharm ambayo inatarajia kuanza kutolewa mkoani Ruvuma Oktoba 25 mwaka huu
Baadhi ya wadau mkoani Ruvuma ambao wameshiriki kikao cha tathmini ya utekelezaji wa mpango wa jamii shirikishi na harakishi wa utoaji chanjo ya UVIKO 19 kilichofanyika kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea
MKOA wa Ruvuma umeongoza kitaifa zoezi la utoaji chanjo ya UVIKO 91
kwa kutoa chanjo kwa watu 44,549 sawa na asilimia 148.5.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert
Ibuge wakati anafungua kikao cha tathmini ya utekelezaji wa mpango wa
jamii shirikishi na harakishi wa utoaji wa chanjo ya UVIKO 19 kilichofanyika
kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea.
“Nitumie nafasi hii kuwapongeza wanaruvuma kwa mwitikio mkubwa
ambao kwa hakika umesababisha Mkoa wetu umeongoza kitaifa’’,alisema
Brigedia Jenerali Ibuge.
Amesema Mkoa wa Ruvuma ulianza rasmi utekelezaji wa chanjo kwa
wananchi Septemba 22 hadi Oktoba 14 mwaka huu,ambapo Mkoa ulivuka
malengo kwa kumaliza dozi 30,000 ulizopewa kwa awamu ya kwanza na
kuongeza dozi nyingine ziada 14,000 hivyo kufikia dozi zaidi ya 44,000.
Hata hivyo amesema tayari serikali ya Tanzania imepokea dozi zaidi ya
milioni moja za chanjo ya UVIKO 19 aina ya sinopharm kwa ajili ya
kuendelea kuwapatia wananchi wake chanjo ambapo Mkoa wa Ruvuma
umeletewa dozi zaidi ya 31,000 ambazo zinatarajiwa kuanza kutolewa kwa
wananchi Oktoba 25 mwaka huu.
Amewaagiza watendaji wa Halmashauri zote mkoani Ruvuma kuhakikisha
wanasambaza chanjo haraka katika vituo vyote 298 vinavyotoa chanjo na
kwamba wataalam wa afya watoe elimu ya chanjo ya sinopharm ili
ifahamike vizuri kwa wananchi kabla ya kuamua kuchanja kwa hiari.
Kwa upande wake Mratibu wa Chanjo Mkoa wa Ruvuma Winbroad Mvile
ameitaja chanjo ya sinopharm kuwa inatolewa mara mbili ili kukamilisha
dozi na kwamba chanjo hiyo inatengeneza kinga dhidi ya UVIKO 19 kwa
asilimia 95.
Akizungumzia mgawanyo wa chanjo hiyo kwa kila Halmashauri mkoani
Ruvuma,Mratibu huyo amesema Mkoa umeletewa dozi zaidi ya 31,291 za
sinopharm ambapo Manispaa ya Songea imepewa dozi 5300,Tunduru
5300,Namtumbo 5300, Halmashauri ya Mbinga 3572,Nyasa 3572,
Halmashauri ya Songea 3572,Mbinga Mji 3572 na Madaba 1103.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Dr.Jairy Kanga
ametoa rai wananchi ambao hawakupata chanjo katika awamu ya kwanza
kujitokeza ili Mkoa wa Ruvuma na Taifa kwa ujumla kufikia hatua ya
kupata kinga kundi (Herd Immunity) ili kufikia asilimia 60 hadi 70 ya watu
wawe wamepata chanjo.
Akizungumzia chanjo ya sinopharm,Dr.Kanga amewataja walengwa wa
chanjo hiyo kuwa ni mtu yeyote mwenye umri wa kuanzia miaka 18 na
kwamba chanjo hii pia inatolewa kwa akinamama wajawazito na
wanaonyonyesha.
Hata hivyo amesema mtu yeyote ambaye hajachanja chanjo ya kwanza ya
Jassen& Jassen anaruhusiwa kupata chanjo ya pili ya sinopharm na
kwamba chanzo zote ni salama na zina uwezo wa kujikinga na UVIKO 19
kwa asilimia 95.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Oktoba 22,2021