Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia Sekta ya Ujenzi, Arch. Elius Mwakalinga, akifungua kikao kazi cha watumishi 44 kutoka katika Sekta hiyo na taasisi zake ambao watashiriki mafunzo kwa vitendo katika miradi ya ujenzi wa miundombinu inayoendelea kutekelezwa hapa nchini
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Huduma ya Ufundi na Umeme kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) Arch. Edwin Nunduma, akifafanua jambo kwenye kikao kazi cha watumishi 44 kutoka katika Sekta hiyo na taasisi zake ambao wamepata fursa ya kushiriki mafunzo kwa vitendo kazini katika miradi ya ujenzi wa miundombinu inayoendelea kutekelezwa hapa nchini.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia Sekta ya Ujenzi, Arch. Elius Mwakalinga, akisaini mkataba wa makubaliano kati ya Serikali na Watumishi kutoka katika Sekta hiyo na taasisi zake kabla ya kwenda kushiriki mafunzo kwa vitendo katika miradi ya ujenzi wa miundombinu inayoendelea kutekelezwa hapa nchini. Kushoto ni Mwanasheria wa Sekta hiyo Bi. Saumu Mruke.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia Sekta ya Ujenzi, Arch. Elius Mwakalinga, akikabidhi hadidu za rejea za mafunzo kwa Mhandisi Gladiness Kitaly kutoka katika Sekta hiyo ambazo zitamsaidia katika mafunzo yake kwa vitendo kazini katika miradi ya ujenzi wa miundombinu inayoendelea kutekelezwa hapa nchini.
Mkadiriaji Majengo kutoka Bodi ya Usajili ya Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB) Joseph Ringo, akitoa neno la shukrani kwa Serikali kwa niaba ya watumishi 44 waliopata fursa ya kushiriki mafunzo kwa vitendo kazini katika miradi ya ujenzi wa miundombinu inayoendelea kutekelezwa hapa nchini.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia Sekta ya Ujenzi, Arch. Elius Mwakalinga, akiwa katika picha ya pamoja na wataalam 44 kutoka katika Wizara hiyo na taasisi zake watakaoshiriki mafunzo yake kwa vitendo katika miradi ya ujenzi wa miundombinu inayoendelea kutekelezwa hapa nchini.
………………..
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kupitia Sekta ya Ujenzi imefanikisha zoezi la kuwapeleka watumishi 44 kushiriki mafunzo kwa vitendo katika miradi ya ujenzi wa miundombinu inayoendelea kutekelezwa hapa nchini.
Mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo watalaamu kutoka katika Wizara hiyo na taasisi zake ili wawe mahiri katika eneo la Ushauri, Ujenzi na Usimamizi wa miradi mikubwa 11 ikiwemo ya barabara, madaraja, viwanja vya ndege na mradi wa kufufua umeme katika Mto Rufiji.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo anayeshughulikia Sekta ya Ujenzi, Arch. Elius Mwakalinga, wakati akifungua kikao kazi cha mafunzo kwa vitendo kazini ambapo pamoja na mambo mengine amesisitiza kwa watumishi hao kujifunza kwa manufaa ya Sekta ya Ujenzi na Taifa kwa ujumla ili kujenga uchumi wa viwanda na hivyo kufanikisha Tanzania kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
“Wote tunafahamu kuwa hivi sasa ni takribani miaka zaidi ya 50 tokea tupate uhuru lakini miradi mingi inaendelea kutekelezwa na wageni hivyo basi mtumie fursa hii mliyopewa kuwa mabalozi wazuri ili nchi iweze kutengeneza makandarasi na washauri elekezi wazawa wengi miaka ya baadae”, amesisitiza Mwakalinga.
Aidha, amewataka watumishi hao kuwa na nidhamu wakiwa katika maeneo yao ya mafunzo na kutokuwa wajuaji bali waongeze ujuzi kwa yale wanayoyajua na kujifunza kwa bidii teknolojia mpya ambazo walikuwa hawazitumii.
Amefafanua kuwa mpango huo utafanyika kwa kipindi cha miezi sita sita na ni moja kati ya mipango ya Wizara iliyojiwekea katika kuhakikisha inaleta chachu ya maendeleo ya nchi hasa katika suala zima la usimamizi na ujenzi wa miundombinu bora.
Arch. Mwakalinga ameeleza kuwa watumishi hao watasaini makubaliano kati ya yao na Mwajiri (on job training bond agreement) na pia kupatiwa vitendea kazi muhimu ili kuwawezesha kujifunza kwa ufanisi.
Kwa upande wake Mtaalam wa Utafiti kutoka Bodi ya Usajili ya Makandarasi (CRB) Arch. Neema Fuime, amesema mafunzo hayo ya watumishi kwa vitendo wakiwa kazini itasaidia fedha nyingi zinazotolewa kwenda kwa makandarasi wageni kubaki hapa nchini na thamani ya fedha kuonekana kwa kuwa wasimamizi na washauri watakuwa ni wazawa wenye uchungu wa nchi yao.
Naye Mkadiriaji Majengo kutoka Bodi ya Usajili na wakadiriaji Majenzi (AQRB) Joseph Ringo, ameishukuru Serikali kupitia Wizara kwa kutoa fursa hiyo kwa watumishi na kumuahidi Katibu Mkuu huyo kushirikiana kikamilifu na wataalam hao na ameahidi kutoinagusha Serikali iliyowaamini katika na kuwapeleka kwenye miradi mikubwa ya kitaifa katika suala la usimamizi, ujenzi na ushauri.
Watumishi hao 44 wamepelekwa mikoa mbalimbali ikiwemo mkoa wa Dar es Salaam, Morogoro, Njombe, Ruvuma na Mtwara ambapo miradi mikubwa ya miundominu ikiendelea kutekelezwa.