Na. Mwandishi Maalum, Addis Ababa
Mkutano wa 39 wa
Kawaida wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi za Umoja wa Afrika umefunguliwa leo
jijini Addis Ababa, Ethiopia ambapo pamoja na mambo mengine, Mawaziri watapitia
Andiko na mikakati ya utekelezaji wa kaulimbiu ya Mwaka 2022 ya “Lishe na
Usalama wa Chakula barani Afrika”. Kaulimbiu hiyo inalenga kusisitiza umuhimu
wa lishe bora kwa ajili ya ukuaji na ustawi wa watoto barani Afrika, bara
ambalo kwa miaka mingi limekuwa linakabiliwa na uzalishaji mdogo wa chakula. Hivyo, nchi za Afrika zinashauriwa kutekeleza
mapendekezo ya Progarmu ya Afrika ya Maendeleo ya Kilimo na Azimio la Malabo
kuhusu kilimo ili kuondokana na changamoto ya lishe duni.
Waziri wa Mambo ya Nje
na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula anaongoza ujumbe
wa Tanzania katika mkutano huo na katika mijadala yake, pamoja na mambo mengine,
anatarajiwa kusisitiza umuhimu wa kukifanya Kiswahili kuwa moja ya lugha ya
kazi katika Umoja wa Afrika.
Mhe. Mulamula atakumbusha
na kulisisitiza suala hilo kwa sababu limeainishwa katika kaulimbiu ya mwaka
2021 ambayo pamoja na mambo mengine, imehimiza matumizi ya lugha za kiafrika na
Kiswahili ni moja ya lugha hizo ambayo inakuwa kwa kasi na kuzungumzwa na watu
wengi barani Afrika na duniani kwa ujumla.
Aidha, Waheshimiwa
Mawaziri watapokea taarifa kuhusu ugonjwa wa UVIKO-19 ambapo katika hotuba ya
ufunguzi ya Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje
wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo alisistiza umuhimu wa nchi wanachama
kuzingatia tahadhari za maambukizi ya UVIKO-19 ikiwa ni pamoja na kuhamasisha
watu wao kupata chanjo ya ugonjwa huo, huku jitihada zikiendelea kuhakikisha
kuwa nchi za Afrika zinapata idadi ya kutosha ya chanjo kwa ajili ya watu wake.
Katika Mkutano huo pia,
Mawaziri wa Mambo ya Nje watapitia na kupitisha bajeti ya Mwaka 2022 ya
Kamisheni ya Umoja wa Afrika na kufanya uchaguzi wa nafasi mbalimbali za
uongozi, zikiwemo za makamishna wawili wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Rais na
Makamu wa Rais wa Chuo Kikuu cha Pan Africa, wajumbe wanne wa Kamisheni ya
Umoja wa Afrika ya Haki za Binadamu na Watu na wajumbe wanne wa Bodi ya Ushauri
ya Afrika ya Kupambana na Rushwa.
Vile vile, Mkutano wa
39 wa Mawaziri utapitia na kupitisha miundo ya taasisi saba za Umoja wa Afrika,
ukiwemo muundo wa Sekretarieti ya Eneo Huru la Biashara barani Afrika ambalo
Tanzania imeridhia Mkataba wake hivi karibuni. Kupitishwa kwa miundo hiyo
itakuwa ni fursa zikiwemo za ajira kwa nchi wanachama, hivyo, Balozi Mulamula
amewataka Watanzania kuzichangamkia, pindi zitakapotangazwa.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (kushoto) na Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia, Bi. Eliza Rwitunga wakiwa katika kikao cha kujiandaa na ujumbe wa Tanzania kabla ya kuingia kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Umoja wa Afrika. |
Ujumbe wa Tanzania katika kikao cha maandalizi na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula |