…………………………………………………………….
Na Angela Msimbira MVOMERO
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Ummy Mwalimu amesema ataunda timu kutoka Ofisi ya Rais – TAMISEMI kuchunguza matumizi ya shilingi milioni 700 zilizotakiwa kujenga bweni na bwalo katika shule ya Sekondari ya Sokoine Memorial katika Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Mkoani Morogoro
Ameyasema hayo wakati akikagua ujenzi wa shule hiyo leo na kusema kuwa hajaridhishwa na matumizi ya fedha zilizopokelewa kwa ajili ya ujenzi wa bweni na bwalo katika shule hiyo
“Sijaridhishwa na matumizi ya fedha shilingi milioni 700 zilizotolewa kwa ajili ya Ujenzi wa bweni na bwalo la shule hiyo, uhalisia hauonekani” amesisitiza Waziri Ummy
Waziri Ummy amesema kuwa wataalam hao watatakiwa kuangalia thamani ya majengo yaliyojengwa wakilinganisha na fedha zilizotumika ili kuweza kutoa ushauri kiasi cha fedha kinachotakiwa kukamilisha majengo hayo.
Aidha amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kuzingatia utaratibu wa matumizi ya fedha za Serikali.