Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu akimpatia Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe Judicar Omary vitendea kazi kutokomeza tatizo la watoto wanaoishi mitaani kwenye maeneo yao, ikiwemo muongozo wa Kitaifa wa kuwaunganisha watoto na familia zao mara baada ya kukamilika kwa Mkutano uliwakutanisha Mkatibu Tawala Mkamanda wa Polisi wa mikoa na wadau kuweka mikakati ya kuondoka na tatizo la watoto wanaoishi mitaani.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu akifunga kikao cha siku mbili cha Wadau kujadili namna ya kutokomeza tatizo la watoto wanaoishi mitaani
Kamishna Utawala na Rasilimali Watu Kamanda wa Jeshi la Polisi Benedict Wakulyamba akichangia jambo wakati wa kikao cha Wadau kujadili namna ya kutokomeza tatizo watoto wanaoishi mitaani kilichofanyika Jijini Dodoma.
Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano Serikali, WAMJW.
***********************************
Na Mwandishi wetu Dodoma
Serikali kwa kushirikiana na Wadau wa kutokomeza watoto wanaoishi mitaani wameazimia kuanza ukaguzi wa magari ya abiria ili kubaini usafirishaji wa watoto kwa lengo la kuzuia ongezeko la watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani.
Hayo yamefikiwa katika kikao cha pamoja cha Makatibu Tawala wa Mikoa, Makamanda wa Polisi na Wadau wanaoshughulika na kutokomeza watoto wanaoishi mitaani, kilichofanyika Jijini Dodoma.
Katika kikao hicho, wamekubaliana kuwa Jeshi la Polisi lianze kutambua watoto wote wanaoishi na kufanya kazi mitaani ili kuwarejesha kwenye familia zao na kuiomba Wakala wa usafirishaji LATRA na Wadau wa usafiri kuweka mfumo madhubuti wa usafirishaji watoto.
Wamesema ukaguzi wa vyombo vya usafiri hautahusisha ubovu tu wa magari bali hadi kwenye Chesesi ili kubaini usafirishaji wa watoto,ikiwezekana kuwekwa utaratibu wa kuandika umri wa wasafiri.
Aidha, Wadau hao wamesisitiza Jamii kuhamasishwa zaidi kuhusu malezi, matunzo na ulinzi ya watoto kupitia mbinu mbalimbali ikiwemo vyombo vya Habari na nyumba za Ibada.
Kwa upande wake Kamishna wa Utawala na Rasilimali watu Kamanda Benedict Wakulyamba ameishukuru Wizara kwa kuwashirikisha wakiwa ni Wadau muhimu katika kumaliza changamoto hiyo kwani Jeshi la Polisi linahusika moja kwa moja na makundi yanayoshughulikiwa na Wizara na jukumu lao ni kuhakikisha wanatoa ushirikiano wa kutosha kutokomeza tatizo hili.
Akihitimisha kikao hicho Katibu Mkuu Dkt. Jingu, amesema kuna kila sababu ya kuwalea watoto vizuri ili kuondokana na changamoto hiyo na kuwahamasisha Wadau wote kuweka nia thabiti ya kupambana na tatizo hilo kikamilifu.
“Tumefikia Maazimio ya jumla ya kila Taasisi na kama yatatekelezwa ipasavyo uwezekano wa kuondokana na changamoto hii ya Watoto waishio katika Mazingira hatarishi ni mkubwa” alisisitiza Dkt Jingu.
Akiwasilisha mada kuhusu haki ya mtoto, Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria kutoka Wizara ya Afya- Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Lucy Saleko alisema Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009 inawataka wazazi kuwajibika kuwalinda watoto wao dhidi ya ukatili na unyanyasaji wa aina yoyote vinginevyo watachukuliwa hatua.