Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi ( Sekta ya Uchukuzi) Bw. Gabriel Migire akisaini makubaliano ya awali ya kuipatia Nchi ya Burundi eneo la Kujenga Bandari kavu, Kwala, mkoani Pwani.
Katibu Mkuu wizara ya Ujenzi na Uchukuzi( Sekta ya Uchukuzi) Bwa.Gabriel Migire (kulia) na Katibu Mkuu Wizara ya Biashara,Uchukuzi, Viwanda na Utalii wa Burundi Bw. Jeremie Banigwaninzigo, wakionyesha hati ya makubaliano ya awali ya kupeana eneo la kujenga Bandari kavu, Kwala, mkoani Pwani, kwa ajili ya nchi ya Burundi.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Dkt. Leonard Chamuriho (wa pili kulia) akiwa kwenye picha ya pamoja na wajumbe kutoka nchi za Tanzania na Burundi, mara baaada ya kufanya kikao cha maandalizi ya Tanzania kuipatia Burundi eneo la kujenga Bandari Kavu eneo la Kwala, mkoani Pwani.
Picha na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
……………………………………………………………
Serikali ya Burundi imeishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuipatia enao la hekta kumi kwa ajili ya kujenga Bandari kavu eneo la Kwala, mkoani Pwani.
Hayo yamesemwa na Balozi wa Burundi nchini Tanzania Bw. Gervais Abayeho, wakati wa kikao cha pamoja kilichowakutanisha Balozi huyo pamoja na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Dkt. Leonard Chamuriho, katika Ofisi za Wizara hiyo zilizopo Mtumba, jijini Dodoma.
Aidha, Balozi Abayeho, ameongeza kuwa kupatikana kwa eneo hilo kutasaidia wafanyabishara wa Burundi kuweza kuhifadhi shehena zao kabla ya kusafirisha kwenda Burundi , na hivyo kusaidia kupunguza gharama za utunzaji wa mizigo yao wanazozipata kwa sasa.
“Nichukue fursa hii kuishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuweza kutupatia eneo hili kwa ajili ya ujenzi wa Bandari Kavu, tunaamini upatikanaji wake utakuwa mkombozi kwa wasafirishaji wetu”, amesema Balozi Abayeho.
Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Dkt.Leonard Chamuriho, amemhakikishia Balozi huyo pamoja na Ujumbe aliokuja nao kutoka nchini Burundi kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kusafirisha mizigo kutoka Bandari ya Dar es Salaama na kupeleka nhini humo.
Chamuriho amefafanua kuwa kwa sasa Bandari ya Dar es Salaam inaendelea kuboreshwa hivyo ufanisi umeongezeka wa kuhudumia mizigo inayoingia na kutoka Bandarini hapo.
Waziri ameongeza kuwa hatua ya serikali kuipa Serikali ya Burundi eneo la kujenga Bandari kavu ni jambo jema ambalo linapelekea kujenga mahusiano mema baina ya nchi hizo mbili.
Naye, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi) Gabriel Migire, amesema kuwa pamoja na Balozi huyo na ujumbe wake, kutembelea Bandari na Reli ya kisasa pia wamesaini kwa pamoja na wajumbe wa Tanzania makubaliano ya awali ya kuwakabidhi eneo la ujenzi wa Bandari Kavu.
Kwa upande wake Balozi wa Tanzania nchini Burundi Dkt. Jilly Maleko, amesema kuwa upatikanaji wa eneo hilo la Bandari kavu kutapelekea wafanyabiashara wa Burundi kutumia bandari ya Dar es Salaam kwa kiwango kikubwa.
Ujumbe zaidi ya watu kumi kutoka nchini Burundi ulipata fursa ya kutembelea miradi mbalimbali inayotekelzwa na Wizara hiyo ikiwemo ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) pamoja na Bandari ya Dar es salaam na Kigoma
Mwisho