Mamlaka
ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imeendelea na zoezi la
kutoa elimu kwa wateja wake wa Jiji la Dar es Salaam na miji ya Pwani juu
ya mabadiliko ya usomaji wa mita za maji na upokeaji wa bili za maji uliofanywa
hivi karibuni.
Hatua
hiyo inatokana na mabadiliko ya usomaji wa mita yaliyofanywa na Mamlaka kutoka
tarehe 1 hadi 15 kwenda tarehe 20 hadi 30 ya kila mwezi.
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti juu ya mabadiliko hayo, wakazi wa Jiji la Dar es Salaam na
baadhi ya mikoa ya Pwani wamepongeza mabadiliko hayo na kusema yamefanyika
wakati muafaka na yataleta tija kwa Mamlaka na Wananchi kwa ujumla.
“Tunaishukuru
DAWASA kwa mabadiliko haya ya usomaji mita kwa tarehe za mwisho wa mwezi, sisi
wananchi tulishasema sana kuhusu kuletewa bili tarehe tofauti tofauti wakati
vipato vyetu vinatofautiana” alisema ndugu Ramadhan Abdul mkazi wa Kinondoni
Shamba.
Zakia
Mrisho mkazi wa kitongoji cha Sanze, wikaya ya Kisarawe anasema mabadiliko hayo
yamewasaidia sana wananchi wanaotegemea vipato vyao mwisho wa mwezi.
“mfano
sisi watumishi wa umma kipato chetu kikuu ni mshahara unalipwa mwisho wa mwezi,
vile DAWASA walikuwa wanatusomea bili na kutuma message muda wowote halikuwa
jambo zuri, tuliishia kugombana nao na wakati mwingine kuleteana vitisho
mbalimbali. Lakini kwa mabadiliko haya tunajua wamesikia kilio chetu na
wakaamua kujirekebisha” alisema bi Zakia.
Kwa
upande wake *Mkurugenzi wa Biashara na huduma kwa wateja DAWASA, Bi
Rithamary Lwabulinda* amesema mabadiliko hayo yaliyofanywa na Mamlaka
yalifanyiwa utafiti wa kina na shirikishi yaliyolenga kuboresha huduma za
majisafi na usafi wa mazingira.
“Mara
kwa mara huwa tunatenga muda wa kuongea na wateja wetu,hivyo mabadiliko haya ni
miongoni mwa sauti za wateja wetu walizotushauri juu ya uboreshaji wa huduma
zetu ili kuweza kuwafikia wengi zaidi” alisema Bibi Lwabulinda