Wakaguzi wa TBS wakielimisha baadhi ya wauzaji wa maduka ya chakula mkoani Morogoro, namna ya kusajili katika mfumo na umuhimu wa kutumia vifungashio sahihi katika bidhaa zao.
Washiriki wa mafunzo kwa wadau wa mafuta ya kula mkoani Morogoro wakifuatilia kwa makini mafunzo hayo.
********************
Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limeendelea kutoa mafunzo maalum kwa wajasiriamali na wafanyabiashara kwa ujumla wanaojishughulisha na sekta ya mafuta ya kula 282 kutoka katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero na Halmashauri ya Mji ya Gairo za mkoani Morogoro.
Mafunzo haya maalum yamewalenga wajasiriamali na wafanyabiashara wanaojishughulisha na uzalishaji, usambazaji na uuzaji wa mafuta ya kula katika masoko ya ndani na ya nje katika mkoa wa Morogoro.
Akimuwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa TBS Dkt. Athuman Y. Ngenya, Meneja wa Utafiti na Mafunzo wa TBS Bw. Hamisi Mwanasala alisema mafunzo haya ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu ya Shirika sambamba na agizo la Serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara kulitaka Shirika kuendesha mafunzo haya maaalum mikoa yote nchini.
Bw. Sudi alisema Serikali inatambua na kuthamini mchango wa wajasiriamali ikiwa ni pamoja na wanaojishughulisha na sekta mafuta ya kula katika kukuza uchumi wa nchi.Hivyo mafunzo haya ni mahsusi kuwajengea uwezo wadau wa mafuta ya kula nchini ili waweze kuzalisha mafuta kwa wingi na yenye ubora unaokidhi matakwa ya viwango vya mafuta ya kula.
“Mafunzo haya yataenda sambamba na utoaji wa elimu maeneo ya kwenye masoko na vituo vya pembezoni mwa barabara ambapo wauzaji wengi wanauza mafuta ya kula” alisisitiza Bw. Sudi.
Kwa upande wake Afisa Udhibiti Ubora wa TBS, Bi Gudila Boniface alisema ili mafuta ya kula yakidhi viwango ni lazima kufuata kanuni za kilimo bora, usindikaji na usafi.
Bi. Gudila alisema kanuni za kilimo bora zinahusisha matumizi ya mbegu bora, kuvuna kwa wakati mazao yalikomaa.
Kwa upande wa kanuni bora za usindikaji kwa mujibu wa Bi. Gudila ni pamoja na kutumia malighafi bora, vifaa vya kusindikia ambavyo havishiki kutu na vilivyoshauriwa na wataalam.
Akizungumzia kanuni bora za usafi, Bi. Gudila alisema wazalishaji wanatakiwa kuhakikisha vifaa vya kuhifadhi mafuta ni safi ikiwa ni pamoja na madumu yanayotumika kuhifadhi mafuta hayo yawe yamesafishwa vizuri pamoja na usafi wa mazingira.
” Vifungashio/Madumu wanayoweka mafuta wahakikishe wameyasafisha vizuri na waweke lebo zinazoeleza bidhaa hizo ni za aina gani,” alisema na kuongeza kwamba haikubaliki kwenye vifungashio ambavyo wazalishaji wanaweka mafuta iwe lebo inayohusu bidhaa nyingine.
Aidha, alisema mafuta ya kula hayatakiwi kuwekwa juani, kwani yanapokuwa juani kuna kemikali zinazozalishwa na zinaweza kusababisha mafuta kuharibika ambayo yakitumiwa na walaji yanaleta athari za kiafya.
Kwa upande wake Afisa Udhibiti Ubora Mwandamizi wa TBS, Bi. Flora Luvanda alitoa wito kwa wadau hao kuthibitisha ubora wa bidhaa zao, kusajili bidhaa za chakula na vipodozi na majengo yanayojihusisha na bidhaa za vyakula na vipodozi.
” Tunatoa wito kwa wadau kuwasiliana na TBS endapo wanakutana na changamoto yeyote wakati wa usajili tutawaelekeza na kuwasaidia mpaka usajili utakapokamilika,” alisema Bi Flora.
Alisema ni muhimu kwa wafanyabishara kusajili bidhaa na majengo ya vyakula na vipodozi kwa mujibu wa sheria ambayo imetokana na mabadiliko ya Sheria ya fedha ya mwaka 2019 iliyohamisha majukumu ya usimamizi wa usalama na ubora wa vyakula na vipodozi kwa TBS kutoka kwa iliyokua Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA).
Alisema usajili wa bidhaa na majengo ya vyakula na vipodozi ni takwa la kisheria na hivyo kwa kufanya hivyo kutawafanya wafanye biashara zao kwa uhuru na uhakika.
Katika mafunzo haya, TBS imewashirikisha watoa mada kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara na Taasisi nyingine ikiwa ni pamoja na Wakala wa Vipimo (WMA), BRELA, Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) pamoja na maafisa kutoka dawati la Halmashauri husika ikijumuisha Afisa Biashara, Afisa Afya na Afisa Maendeleo ya Jamii.
Mafunzo haya maalum kwa wadau wa mafuta ya kula mkoani Morogoro ni mwendelezo wa mafunzo kama haya yaliyokwisha kutolewa katika mikoa ya Dodoma, Singida, Tabora, Kigoma, Iringa, Njombe, Mbeya na Songwe.