Ofisa Misitu wa Wilaya ya Mbinga Halifa Singano akichuma uyoga kwenye Msitu wa Kijiji cha Amani Makoro wilayani Mbinga mkoani Ruvuma.
Wakina mama wachuma uyoga asili Hilda Komba (katikati) Veronica Sakwaya (kulia) na Germana Clement wa kwanza kushoto, kutoka kijiji cha Amani Makoro kata ya Amani Makoro wilayani Mbinga mkoani Ruvuma wakichuma na kuandaa uyoga kwenye msitu wa kijiji.
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Amani Makoro, Joachim Kaponda akielezea namna program ya FORVAC inavyochangia maendeleo na uhifadhi.
Mratibu wa FORVAC Kongani ya Ruvuma, Marcel Mutunda akielezea namn program hiyo inachakata kupata vikundi vya kusaidiwa.
*******************************************
NA SULEIMAN MSUYA, MBINGA
VIKUNDI na watu binafsi vipatavyo 20 kutoka katika vijiji saba vya wilayani Mbinga mkoani Ruvuma wamepatiwa vifaa vya kuongeza mnyororo wa thamani wa mazao ya misitu vyenye thamani ya shilingi milioni 100.
Hayo yamesemwa na Mtaribu wa FORVAC, Kongani ya Ruvuma, yenye wilaya za Nyasa, Mbinga, Namtumbo, Songea na Tunduru, Marcel Mutunda wakati akizungumza na mwandishi wa habari hii.
Mutunda amesema FORVAC inatekelezwa na Idara ya Misitu na Nyuki kupitia ufadhili wa Serikali ya Tanzania na Finland ina lengo la kuhakikisha mazao ya misitu yanakuwa kwenye mnyororo wa thamani na kuwanufaisha wanavijiji.
Amesema wamewezesha vikundi na watu binafsi vipatavyo 20 katika Wilaya ya Mbinga kushiriki kwenye uhifadhi wa misitu kwa kuwekeza mizinga ya nyuki, kuokota uyoga na wasusi wa makapu na nyungo hivyo vifaa vya kuchakata mazao ya misitu vitaongeza thamani.
“Kwa mwaka huu FORVAC imetoa shilingi milioni 100 kwa vikundi 20 ili wanununua vifaa vya kuchakata uyoga, nyuki, nta, asali, makapu na nyungo ambapo tumeingia mkataba na Sedet Vicoba ili wanunue vifaa hivyo.
Mfano hapa katika kijiji cha Amani Makoro wanavikundi wameomba mitambo ya kurina na kukamukia asali kama buti, nguo, chujio na vingine,” amesema.
Mtatibu huyo amesema pia wametoa pikipiki moja kwa Mzee Komba ambaye anajihusisha na kuchukua mianzi ili atengeneze makapu na nyungo.
Amesema wamewawezesha wakina mama watatu ambao wanajihusisha na uokotoji wa uyoga ambao wamepatiwa mitambo ya kuchakata uyoga, nguo na buti ili kujikinga na wadudu wabaya kama nyoka.
Amesema vikundi vingine ambavyo vitapata vitendeakazi ni pamoja na Kijiji cha Ukata, Kiwombi, Kindimba Juu, Kindimba Chini, Ndongosi na Barabara.
Akizungumzia ujio wa FORVAC wilayani Mbinga Ofisa Misitu wa wilaya hiyo Halifa Singano amesema program hiyo ina tija kwa jamii.
Singano amesema kupitia program hiyo jamii imeinuka kiuchumi kwa kuwa wanatumia misitu kuvuna mazao ambayo sio mbao kwa njia endelevu.
Amesema FORVAC imechochea uhifadhi, kuzuia uvunaji haramu na kuwafanya wananchi kutambua faida za misitu.
Ofisa misitu huyo amesema katika kuhakikisha dhana ya FORVAC inasambaa wameendelea kutoa elimu kwa wanavijiji kuunda vikundi ili wapate fedha za halmashauri kusimamia misitu.
“FORVAC imeleta mabadiliko makubwa ya kifikra kuhusu uhifadhi hivyo sisi tutaendelea kutoa elimu ili vikundi na watu binafsi kushiriki katika kulinda na kutunza misitu,” amesema.
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Amani Makoro, Joachim Kaponda amesema program hiyo imekuja wakati muafaka kwani misitu imeanza kulindwa.
“Ujio wa FORVAC umeibua vikundi vinne vya Hapa Kazi Tu, Jitambue na vingine hapa Amani Makoro ambavyo vinajihusisha na ufugaji wa nyuki na vingine vinachuma uyoga hali ambayo inasadia wanakijiji kuwa na shughuli nyingi za kufanya tofauti na zamani,” amesema.
Amesema wanaiomba FORVAC kuendelea kutoa elimu ili wanavijiji wengi kujiunga na program hiyo muhimu ambayo itachangia ongezeko la kipato kwa wanavijiji na Serikali.
Diwani wa Kata ya Amani Makoro Ambros Nchimbi, amesema program hiyo imepunguza utegemezi kwa wananchi wengi wa kata yake jambo ambalo linamrahisishia ufanyaji kazi.
“Nina vijiji viwili vya Amani Makoro na Kiwombi ambao vinatumia msitu wa asili inayowazunguka kutekeleza shughuli zao,” amesema
Wakizungumzia ujio wa FORVAC wachuma uyoga asili Hilda Komba, Veronica Sakwaya na Germana Clement wamesema program hiyo imeweza kubadilisha maisha yao kiuchumi, kijamii na maendeleo.
Wamesema kupitia uchumaji wa uyoga asili wameweza kufanikisha mipango yao mingi bila kuwa wategemezi kwa waume zao.
“Sisi uyoga ni mkomboazi wa maisha yetu umetuondolea utegemezi tunawapongeza sana FORVAC kwa kutuwezesha,” amesema.
Naye Jackson Boimanda Mshauri wa Masuala ya Biashara kutoa Shirika la Sedet amesema wao wamekuwa wakitoa elimu kwa vikundi ili kujua namna ya kufikia malengo.
Amesema wanavijiji waliopo kwenye vikundi wameonesha uelewa katika kuomba fedha na vifaa jambo ambalo linawapa faraja.