Afisa Udhibiti ubora, Bi Matrona Emmanuel (TBS) akitoa elimu kwa wadau mbalimbali waliotembelea banda la TBS kwenye maonesho ya wafanyabiashara wanawake yanayoendelea katikaViwanja vya Mlimani City jijini Dar- es- salaam.
********************************************
SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limewataka wafanyabiashara kujitokeza kusajili bidhaa, majengo ya vyakula na vipodozi ili kuwawezesha kufanya shughuli zao kwa kukidhi matakwa ya sheria za nchi na kulinda afya za walaji.
Wito huo umetolewa na afisa uhusiano wa TBS, Bi. Neema Mtemvu kwenye Maonesho ya wafanyabiashara wanawake Tanzania yaliyoanza Machi 4, mwaka huu hadi Machi 7 jijini Dar es salaam katika Viwanja vya Mlimani City.
Shirika hilo linashiriki maonesho hayo kwa ajili ya kutoa elimu ya viwango kwa wananchi, wajasiriamali, wafanyabiashara na wadau mbalimbali na msisitizo wao mkubwa ni ujenzi wa Tanzania ya viwanda na kukua kiuchumi.
“Tunatoa wito kwa wanaofika kwenye maonesho haya kusajili bidhaa na majengo ya vyakula na vipodozi kwa mujibu wa sheria ambayo imetokana na mabadiliko ya Sheria ya Fedha ya Mwaka 2019,” alisema Mtemvu.
Sheria hiyo ilirudisha majukumu ya usimamizi wa usalama na ubora wa vyakula na vipodozi kwa TBS kutoka kwa iliyokuwa Mamlaka ya Dawa na Chakula Tanzania (TFDA).
“Kwa hiyo usajili wa bidhaa, majengo ya vyakula na vipodozi ni takwa la kisheria ili kuwawezesha kufanyabiashara zao urahisi,” alisema Mtemvu wakati akitoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali kwa wananchi waliotembelea banda la shirika hilo kwenye maonesho hayo.
Alisema usajili majengo ya biashara unawapa wafanyabiashara uhakika wa kutunza bidhaa na kwamba wanasajili jengo kulingana na bidhaa zinazoenda kuhifadhiwa humo.
Kwa upande wa usajili wa bidhaa, Mtemvu alisema eneo linalohusika ni bidhaa za chakula na vipodozi zinazoingizwa nchini kutoka nje ya nchi.
Alisema usajili wa vipodozi unalenga kuhakikisha vipodozi vilivyopigwa marufuku kwenye soko la Tanzania haviingizwi nchini kutokana na kuwa na viambata sumu.
Wakati huo huo, Mtemvu ametoa wito kwa wajasiriamali kujitokeza kwa wingi kuthibitisha ubora wa bidhaa zao TBS bure, kwani gharama hizo zinalipwa na Serikali kwa lengo la kuwawezesha kufanyabiashara.
Alisema wanachotakiwa kuwa nacho ni barua ya utambulisho kutoka SIDO na baada ya hapo wakifika TBS mchakato unaanza mara mara moja. Alisema wamefurahishwa na mwitikio mkubwa wa wananchi kwenye maonesho hayo.