Jengo la vyumba viwili vya madarasa na ofisi moja ya Walimu katika shule ya Sekondari Magingo Halmashauri ya wilaya Madaba mkoani Ruvuma ambalo limekamilika na limeanza kutumika na wanafunzi wa shule hiyo ambalo limejengwa kwa lengo la kumaliza msongamano wa wanafunzi madarasani.
***************************************
Na Muhidin Amri,
Madaba
HALMASHAURI ya Madaba wilayani Songea, imefanikiwa kupeleka watoto wote 1148,waliofanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka jana na kuchaguliwa kuanza elimu ya sekondari katika muhula wa masomo 2021 kwenye shule walizopangiwa.
Akizungumza na Habarileo ofisini kwake, Afisa Elimu sekondari wa Halmashauri hiyo Michael Hadu alisema, wamefanikiwa kupeleka watoto wote walio kuchaguliwa kuendelea na elimu ya sekondari mwaka huu baada ya kukamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa.
Hadu alisema, kati ya wanafunzi hao wavulana 585 na Wasichana 563 ambapo wanafunzi 10 wamechaguliwa kwenda katika shule mbalimbali za Bweni za serikali zilizopo nje ya Halmashauri ya Madaba.
“ katika Halmashauri yetu ya Madaba tumefaulisha wanafunzi 1148 na wote wamepata nafasi ya kujiunga na kidato cha kwanza kwenye shule walizopangiwa na hakuna mwanafunzi aliyekosa nafasi na wote wako shuleni”alisema Hadu.
Alisema, Rais Dkt John Magufuli ameweka dhamira ya dhati ya kutoa elimu bure, na Halmashauri imehakikisha wanafunzi wote waliochaguliwa wanaendelea na elimu ya sekondari ambapo ameipongeza Serikali kwa kutoa fedha za kujenga madarasa mapya kwa ajili ya wanafunzi hao.
Kwa upande wa vyumba vya madarasa alisema, mahitaji kwa wanafunzi hao ilikuwa 25 na wakati wanachaguliwa kulikuwa na vyumba 23 hivyo kuwa na upungufu wa vyumba 2,hata hivyo darasa moja limekamilika lililojengwa kwa ushirikiano kati ya wananchi na Halmashauri.
Alisema,darasa lingine lipo katika hatua ya boma ambapo Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya imeshatoa kiasi cha shilingi milioni 6 ili kukamilisha ujenzi wake.
Kuhusu mahitaji ya viti kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka 2021 ilikuwa 1148,vilivyokuwepo 987 na pungufu 161,mahitaji ya meza 1148 zilizowepo 976 hivyo kuwa na upungufu wa meza 172.
Hata hivyo, kutokana na uhusiano mzuri kati ya Halmashauri na wadau mbalimbali, ikiwemo Benki ya NMB Tawi la Madaba iliyotengeneza viti 50 na meza 50 na Halmashauri imetoa shilingi milioni 10 ambazo zimesaidia kumaliza upungufu huo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Shafi Mpenda, ameishukuru Serikali kwa kutoa fedha ambazo zimetumika kuboresha sekta ya elimu mwaka hadi mwaka.
Alisema, Serikali imetoa kiasi cha shilingi milioni 299.678 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya P4R kwa kujenga vyumba vya madarasa,matundu ya choo kwa baadhi ya shule.
Alieleza kuwa,changamoto kubwa katika utekelezaji wa miradi ni kuchelewa kwa vifungu vya matumizi ya fedha,saruji kutopatikana kwa wakati,ukiukaji wa maadili katika matumizi ya fedha na uzembe kwa walimu uliosababisha baadhi ya miradi kuchelewa kukamilika.
Alisema, kutokana na kasoro hizo amelazimika kuwavua madaraka walimu waliofanya uzembe na kutumia fedha hizo vibaya, na hatua hiyo inalenga kujenga nidhamu juu ya matumizi ya fedha za miradi.
Mpenda alitoa mfano wa Mkuu wa shule ya Sekondari Gumbiro aliyemlipa fedha nyingi fundi aliyepewa kazi ya kujenga matundu ya vyoo katika shule hiyo kupitia fedha za mradi wa ujenzi wa vyoo bora unaofahamika kwa jina la Swash kuliko kazi iliyofanyika ambapo amemtaka Mwalimu huyo kumalizia kazi hiyo kwa gharama zake.
Katika hatua nyingine Mpenda alisema, Halmashauri hiyo imetekeleza agizo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa lililowataka Wakurugenzi wa Halmashauri za wilaya,miji,Manispaa na Majiji kumaliza ujenzi wa vyumba vya madarasa, madawati na viti kwenye shule za sekondari ifikapo tarehe 28 Mwezi uliopita.
Mpenda alibainisha kuwa, Halmashauri kwa kushirikiana na wadau wengine wa elimu imekamilisha agizo hilo kwa asilimia 100 na hakuna mtoto anayekaa chini kwa kukosa kiti na meza au kusoma chini ya miti.