Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile akizungumza na wafanyakazi wa Wizara yake (hawapo pichani) wakati wa kikao chake na wafanyakazi hao, Dodoma. Wa kwanza kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Zainab Chaula na wa pili kulia ni Naibu Katibu Mkuu, Dkt. Jim Yonazi na anayesikiliza kwa makini ni Mwenyekiti wa TUGHE wa Wizara hiyo, Laurencia Masigo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Zainab Chaula akisisitiza jambo kwa wafanyakazi wa Wizara hiyo (hawapo pichani) kabla ya kikao cha wafanyakazi wa Wizara hiyo na Waziri wao, Dkt. Faustine Ndugulile (wa pili kushoto) kilichofanyika Dodoma
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Jim Yonazi, akitoa neno la shukrani baada ya kikao cha Waziri wa Wizara hiyo, Dkt. Faustine Ndugulile (wa pili kushoto) na wafanyakazi wa Wizara hiyo (hawapo pichani). Wa kwanza kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Zainab Chaula na wa kwanza kulia ni Mwenyekiti wa TUGHE, Wizarani hapo, Laurencia Masigo
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile (wa pili kushoto) akimpongeza dereva wa kike pekee wa Wizara hiyo, Trust Kyando kwa utendaji kazi mzuri wakati wa kikao cha Waziri huyo na wafanyakazi wa Wizara hiyo. Wa kwanza kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Zainab Chaula
Mwenyekiti wa TUGHE wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Laurencia Masigo (wa kwanza kulia) akiongoza wafanyakazi wa Wizara hiyo kuimba wimbo wa Wafanyakazi Tujiunge Pamoja wakati wa kikao cha Waziri wa Wizara hiyo, Dkt. Faustine Ndugulile (anayeimba katikati) wakati wa kikao chake na wafanyakazi hao, Dodoma.
*********************************************
- Awataka watumie TEHAMA kutatua changamoto za wananchi
- Asema Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ni Barabara ya Dunia ya Sasa ya Kidijitali
- TAwataka Wahakikishe TEHAMA Inachangia Kikamilifu Pato la Taifa
Na Prisca Ulomi, WMTH
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile amewataka wafanyakazi wa Wizara yake kuacha kufanya kazi kwa mazoea badala yake wafanye kazi kwa ubunifu, kujituma, watumie TEHAMA kutatua changamoto za wananchi, wahakikishe TEHAMA inachangia kikamilifu pato la taifa kwa kuwa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ni barabara ya dunia ya sasa ya kidijitali
Dkt. Ndugulile ameyasema hayo wakati wa kikao chake na wafanyakazi wa Wizara hiyo kilichofanyika Dodoma na kuhudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Zainab Chaula, Naibu Katibu Mkuu, Dkt. Jim Yonazi na wajumbe wa Menejimenti ya Wizara hiyo mpya
Amewataka wafanyakazi hao kuacha kufanya kazi kwa mazoea na yeye sio muumini wa michakato bali anahitaji kuona matokeo ili kuhakikisha kuwa TEHAMA inatumika kujibu changamato za wananchi ili mwananchi apate huduma za Serikali mahali popote alipo badala ya kufuata watendaji walipo
“Nataka kuona bwana shamba anatumia mawasiliano kupata mbegu, pembejeo na wakulima watumie TEHAMA kupata masoko, waalimu tulionao watumie TEHAMA kufundishia wanafunzi kwa kuwa Wizara hii ina dhamana na masuala ya TEHAMA, ndiyo yenye sera ya TEHAMA, inatoa miongozo, sheria, kanuni na viwango kwa taasisi zote za Serikali, sekta binafsi na wananchi”, amesisitiza Dkt. Ndugulile
Amefafanua kuwa sasa hivi Serikali inatumia fedha nyingi kununua mifumo ya TEHAMA nje ya nchi, hivyo anataka wabunifu wa TEHAMA wazuri waliopo nchini watumike kutengeneza mitandao yetu ya kijamii na mifumo yetu ya TEHAMA ambayo ina jibu changamoto za wananchi ili Tanzania tuwe na mitandao yetu na mifumo yetu ya TEHAMA ili kuongeza pato la Taifa
Katibu Mkuu wa Wizara, Dkt. Zainab Chaula amesema kuwa kikao hicho kitawawezesha wafanyakazi kuwa na dira na mwelekeo wa pamoja katika kutekeleza majukumju ya Wizara mpya na Naibu Katibu Mkuu, Dkt. Jim Yonazi amemshukuru Waziri kwa kikao hicho na kuongeza ari kwa wafanyakazi kutumikia wananchi
Naye Mwenyekiti wa TUGHE wa Wizara hiyo, Laurencia Masigo amemweleza Dkt. Ndugulile kuwa wafanyakazi wako tayari kufanya kazi kwa ushirikiano, kujituma na kushirikiana na Menejimenti na kushauri yapi yafanyike katika nyanja ya TEHAMA ili kukuza uchumi wa taifa letu