*Asema imejipanga kuongeza uwezo wa uzalishaji umeme na kufikia megawati 8,000
*Aeleza Serikali inatambua mchango wa TANESCO katika kufanikisha ukuaji wa viwanda, uwekezaji na huduma zakijamii.
Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Dkt. Juma Homera, amesema Serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) katika kuimarisha upatikanaji wa umeme hatua ambayo imekuwa chachu ya ukuaji wa viwanda, uwekezaji na maendeleo ya huduma za kijamii.
Amesema TANESCO, kwa kushirikiana na wadau , imejipanga kuongeza uwezo wa uzalishaji umeme kupitia vyanzo mbalimbali ikiwa na matarajio ya kufikisha jumla ya megawati 8,000 ifikapo mwaka 2030. Hatua hiyo inalenga kukidhi mahitaji ya umeme yanayoendelea kuongezeka.
Waziri Homera ameyasema hayo leo, Novemba 26, 2026, wakati TANESCO ikiadhimisha miaka 95 tangu kuanzishwa kwake, akieleza kuwa ni safari ya kihistoria iliyobeba maono, changamoto, mafanikio na ubunifu mkubwa katika kujenga uchumi wa Tanzania kupitia nishati ya umeme.
Amesema katika kipindi ambacho Taifa linaendelea kutekeleza Dira ya Maendeleo ya mwaka 2050, TANESCO inatambulika kama chombo muhimu katika kufanikisha mageuzi ya kiuchumi kupitia uwekezaji
Waziri Homera ameipongeza Bodi ya Wakurugenzi, Menejimenti na wafanyakazi wa TANESCO kwa uzalendo, kujituma na mchango wao katika kuhakikisha huduma ya umeme nchini inaendelea kuimarika.
“Naipongeza Bodi na Menejimenti ya TANESCO kwa kazi kubwa ya kuhakikisha umeme unawafikia watanzania, TANESCO inampango wa kuongeza uwezo wa uzalishaji umeme hadi kufikia Megati 8,000 mwaka 2030. Hatua hii inalenga kukidhi mahitaji ya umeme yanaoendelea kuongezeka na kuendelea kuwa chombo muhimu katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii’’Alisema Mhe. Homera
Amesisitiza umuhimu wa kuendelea kutumia mifumo ya kisasa ya teknolojia katika utoaji wa huduma za umeme ili kurahisisha upatikanaji wa huduma hizo kwa wananchi wengi zaidi na kuongeza ufanisi katika shughuli za Shirika.
Shirika la umeme Tanzania (TANESCO) leo linaadhimisha miaka 95 tangu kuanzishwa kwake tarehe 26 Novemba 1991 likiwa linajivunia kupiga hatua kubwa katika shughuli za uzalishaji, usafirishaji na usambazaji umeme nchini.
