Na Mwamvua Mwinyi, Pwani

KAMISHNA Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Juma Mwenda, amesema mapambano dhidi ya magendo ni hatua muhimu katika kulinda biashara halali, kuhakikisha wafanyabiashara wanaofuata sheria wanapata mazingira sawa ya ushindani na kulinda maslahi ya walipakodi waaminifu.

Mwenda ameyasema hayo wakati wa ziara yake ya kutembelea Ofisi za TRA Mkoa wa Pwani, ambapo alikutana na watumishi na kusisitiza umuhimu wa kuimarisha ufanisi katika usimamizi wa kodi pamoja na kudhibiti vitendo vya magendo.

Amesema mapambano dhidi ya magendo si suala la kudhibiti bidhaa zinazoingizwa au kusafirishwa nchini kinyume cha sheria pekee, bali pia ni sehemu ya kuhakikisha wafanyabiashara wanaotimiza wajibu wao kwa Serikali hawakabiliwi na ushindani usio wa haki unaotokana na biashara haramu.

Aidha, amewahimiza watumishi wa TRA kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uadilifu na uwajibikaji, huku wakizingatia haki za walipakodi na kuhakikisha usimamizi wa kodi unakwenda sambamba na kujenga mazingira rafiki ya biashara na kuchochea maendeleo ya uchumi wa Taifa