Na Mwandishi wetu, Simanjiro

KAMPUNI ya uchimbaji madini ya Tanzanite Africa inayofanya shughuli zake eneo la kitalu D Extension imewapatia mradi wa maji zaidi ya watu 200 wa kitongoji cha Katikati Kijiji cha Naisinyai Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara.

Wakazi wa eneo hilo waliokuwa wanatembea umbali mrefu wa kilomita 25 kufuata maji wameondoka na changamoto hiyo baada ya kukabidhiwa chanzo cha mradi huo wa maji na kampuni hiyo ya Tanzanite Africa.

Mkurugenzi wa kampuni ya Tanzanite Africa LTD, Wilfred Mushi amesema baada ya kuombwa kuwapatia maji wananchi wa eneo hilo alitekeleza ombi hilo kutokana na kusikia kero wanayoipata wakazi wa eneo hilo.

Mushi amesema baada ya watu wa eneo hilo kupata maji hivi sasa atawapatia wananchi hao tenki lingine lenye uwezo wa kuhifadhi lita 10,0000 za maji.

“Pia mwezi Januari mwaka 2026 kampuni yetu ya Tanzanite Africa LTD, tunatarajia kutoa nafasi 10 za ajira ila tutawapatia nafasi tano wananchi wa kijiji hiki cha Naisinyai,” amesema Mushi.

Mwenyekiti wa kijiji cha Naisinyai Joseph Maliaki akizungumza kwenye uzinduzi wa mradi huo uliowezeshwa na kampuni ya Tanzanite Africa, amesema jamii ya eneo hilo na mifugo waliteseka kupata maji.

Maliaki amesema wanaishukuru kampuni ya Tanzanite Africa kwa kuwapatia chanzo cha maji ambacho ndicho watu wa kitongoji hicho na mifugo yao wanatumia hivi sasa.

Mwenyekiti wa jumuiya ya umoja wa vijana (UVCCM) Patimayo Mollel akisoma taarifa ya mradi huo amesema watu 200 na mifugo watanufaika nao.

Mollel amesema mradi huo umetekelezwa na kampuni ya Tanzanite Africa kwa kutoa chanjo cha maji na kampuni ya Franone Mining kwa kutoa tenki la maji lenye ujazo wa lita 10,000.

Amesema mbunge wa Simanjiro James Ole Millya amechangia rola moja ya bomba, wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini RUWASA Wilayani Simanjiro wamechangia rola mbili za bomba la maji.

“Pia wananchi wa kijiji cha Naisinyai walichanga na kununua rola sita za mabomba ya kupitishia maji, kuchimba mtaro na kumlipa fundi wa ujenzi wa mradi huo,” amesema Mollel.