Qingdao, China.

Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera (Mb.), ametoa wito kwa wawekezaji kutoka China, nchi washiriki wa Mkutano wa Belt and Road Energy Partnership, taasisi za maendeleo na sekta binafsi kuchangamkia fursa za uwekezaji katika sekta ya nishati nchini Tanzania, akisisitiza kuwa milango ya uwekezaji iko wazi kutokana na amani, sera, sheria na kanuni zinazotabirika.  

Amezungumza hayo leo Novemba 26, 2026, katika Mkutano wa Nne wa Mawaziri wa Nishati wa Ukanda Mmoja na Njia Moja (Fourth Belt and Road Energy Ministerial Conference) uliofanyika jijini Qingdao, jimbo la Shandong, Jamhuri ya Watu wa China.

Mhe. Dkt. Homera amebainisha kuwa nishati ni kichocheo cha kimkakati cha ujenzi wa viwanda, mabadiliko ya kiuchumi, utoaji ajira na kuboresha maisha ya wananchi. 

Ameongeza kuwa Tanzania ina utajiri wa rasilimali mbalimbali za nishati ikiwemo gesi asilia, maji, jua, upepo, jotoardhi, urani, makaa ya mawe na haidrojeni, pamoja na nafasi nzuri ya kijiografia inayoiwezesha kuwa kitovu cha nishati katika Afrika Mashariki na Kusini na lango kwa nchi zisizo na bahari.  

Mhe. Dkt. Homera ameeleza kuwa akiba ya gesi asilia nchini imefikia futi za ujazo trilioni 57.54, huku ugunduzi mpya katika vitalu vya Mnazi Bay ukikadiriwa kuwa na futi za ujazo bilioni 223, Hali hii inatoa fursa za kusambaza gesi majumbani na nchi jirani, kupanua vituo vya gesi iliyoshindiliwa (CNG), mini-LNG na gesi kwa ajili ya viwanda. 

Pia amebainisha kuwa hivi karibuni Serikali imetoa leseni nne za utafutaji mafuta kwa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na kuhimiza ushirikiano kama uliopo kati ya TPDC na China National Offshore Oil Corporation (CNOOC) katika mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) uendelezwe katika shughuli za utafutaji wa juu (upstream). 

Aidha, amesisitiza kuwa Tanzania inaongoza Barani Afrika katika ajenda ya nishati safi ya kupikia chini ya uongozi wa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ikilenga kuhakikisha angalau asilimia 80 ya Watanzania wanapata teknolojia ya nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2030, jambo linalofungua fursa za ubunifu na usambazaji wa majiko na teknolojia nafuu nchini kote.