Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

SERIKALI imelielekeza Shirika la Posta Tanzania kutumia ipasavyo vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) vilivyokabidhiwa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) ili kuboresha mifumo ya utoaji huduma, kuongeza ufanisi na kwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia pamoja na mahitaji ya uchumi wa kidijitali.

Wito huo umetolewa jijini Dar es Salaam Novemba 26, 2026, na Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Switbert Mkama, wakati wa hafla ya kukabidhi vifaa hivyo. Amesema mashirika ya posta duniani yanabadilika kutoka katika mfumo wa kusafirisha barua pekee na kuwa vituo vinavyotoa huduma mbalimbali za kidijitali, biashara mtandao, huduma za kifedha na Serikali mtandao.

Amesema mabadiliko hayo yanapaswa kuwa chachu kwa Tanzania kutumia mtandao mpana wa Shirika la Posta, unaofika maeneo mbalimbali kuanzia mijini hadi vijijini, kuharakisha upatikanaji wa huduma za kidijitali na kuhakikisha wananchi wengi zaidi wananufaika na maendeleo ya teknolojia.

Aidha, ameeleza kuwa uwekezaji katika vifaa vya TEHAMA ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kujenga uchumi wa kisasa na shindani unaotegemea maarifa, ubunifu na teknolojia.

Ameongeza kuwa hatua hiyo inaendana na vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Sita vya kujenga Tanzania ya kidijitali, huku akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuimarisha sekta ya posta na mawasiliano ili ziwe na mchango mkubwa katika kukuza maendeleo ya kijamii na kiuchumi na kuwawezesha wananchi kunufaika na fursa zinazotokana na teknolojia za kisasa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa UCSAF, Mlembwa Mnakua, amesema katika kipindi cha miaka minne kuanzia mwaka 2023 hadi mwaka uliopita wa fedha, mfuko huo umewezesha ununuzi wa vifaa vya Shirika la Posta Tanzania vyenye thamani ya Sh bilioni 2.5.

Amesema katika mwaka wa fedha 2026/2027, UCSAF imetenga Sh bilioni 1.8 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya TEHAMA pamoja na kuanzisha vituo vipya vya kutolea huduma za posta, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kusogeza huduma hizo karibu zaidi na wananchi.

Naye Posta Masta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Macrice Mbodo, amesema shirika hilo limejipanga kuhakikisha vifaa vilivyokabidhiwa vinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma na kuleta manufaa kwa wananchi.

Amesema shirika hilo linatambua umuhimu wa kuboresha huduma zake, hususan katika maeneo ya vijijini ambako bado kuna changamoto ya upatikanaji wa huduma, hivyo matumizi sahihi ya vifaa hivyo yatasaidia kupanua wigo wa huduma na kuzisogeza karibu zaidi na wananchi.