Chombo cha anga cha China cha Shenzhou-24, chenye wanaanga, kimefanikiwa kuingia katika obiti iliyokusudiwa baada ya kurushwa kwa mafanikio kutoka Kituo cha Kurushia Satelaiti cha Jiuquan, kaskazini-magharibi mwa China, Jumatano asubuhi.
Chombo hicho, kilichobebwa na roketi ya Long March-2F, kilirushwa Jumatano saa 8:18 asubuhi kwa saa za Beijing.
Takriban dakika 10 baadaye, chombo hicho kilijitenga na roketi na kuingia katika obiti iliyokusudiwa, kikijiandaa kwa hatua ya kuunganishwa na kituo cha anga cha Tiangong.
Wanaanga watatu waliomo kwenye misheni hiyo, akiwemo kamanda Tang Hongbo, mhandisi wa safari za anga Wu Yi na mtaalamu wa mizigo kutoka Pakistan Muhammad Zeeshan Ali, wameripoti kuwa katika hali nzuri, huku Li Benqi kutoka kituo cha kurushia akitangaza kuwa urushaji huo umefanikiwa kikamilifu.
Tang amesema maandalizi ya usalama kwa wanaanga wote ni muhimu katika kuhakikisha mafanikio ya misheni hiyo.
“Nimeweka masharti ya wazi kuhusu kila kitu ambacho anaweza kukutana nacho. Ninamweleza kuwa haya ni masharti kwa sababu yanahusu usalama. Sote tuko ndani ya chombo hicho hicho cha anga, na ili kuhakikisha usalama wa kila mmoja, ni lazima uwe na uelewa na uwezo wa kufanya mambo hayo. Hali hiyo inatuhusu pia sisi. Kuna zaidi ya taratibu 100 za usalama ambazo ni muhimu sana na zinazotumika mara kwa mara,” amesema Tang.
Baada ya kuingia katika obiti, chombo cha Shenzhou-24 kitafanya mchakato wa kukutana na kuunganishwa na kituo cha anga kwa njia ya haraka na ya kiotomatiki, kikielekea kwenye moduli kuu ya kituo hicho cha Tiangong, inayojulikana kama Tianhe.
Misheni hiyo inaashiria safari ya kwanza ya pamoja inayohusisha wanaanga wa China na nchi nyingine katika historia ya mpango wa China wa safari za anga za binadamu.
Mtaalamu wa mizigo kutoka Pakistan, Ali, amesema amejifunza mengi kutoka kwa kamanda Tang Hongbo, akieleza kuwa licha ya uzoefu mkubwa wa kamanda huyo, amekuwa mnyenyekevu na tayari kushiriki maarifa yake.
“Kwanza kabisa, ni kamanda Tang. Nilipofika hapa na kuanza mafunzo pamoja naye, nilikuwa na taswira tofauti sana kumhusu, nikidhani angekuwa mkali sana. Lakini kadiri muda ulivyopita, niligundua kuwa ndiye mtu mnyenyekevu zaidi, licha ya kuwa kamanda mwenye uzoefu mkubwa na aliyekwisha kwenda kwenye kituo hiki cha anga mara mbili. Nilijua pia kuwa safari hii angekuwa kamanda wa kwanza wa kikosi cha kwanza cha kimataifa, lakini bado alikuwa mnyenyekevu sana. Alinifundisha kila kitu alichokuwa amejifunza na uzoefu aliokuwa nao,” amesema Ali.
Mwanaanga huyo wa Pakistan atarejea duniani akiwa ndani ya chombo cha Shenzhou-23 baada ya kukamilisha kipindi kifupi cha kukaa katika kituo cha anga cha China, wakati wa mchakato wa kukabidhiana majukumu kati ya vikosi vya wanaanga.
Mmoja wa wanaanga wa Shenzhou-23, Zhu Yangzhu, atabaki katika kituo cha anga cha Tiangong kukamilisha kipindi cha mwaka mmoja akiwa katika obiti, muda ambao ni mara mbili ya kipindi cha kawaida cha kukaa angani kwa wanaanga katika misheni zilizopita za Shenzhou.
