Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imeandika historia mpya kwa kushika nafasi ya kwanza katika usimamizi bora wa fedha miongoni mwa mashirika ya umma, hatua iliyoiwezesha kutunukiwa tuzo ya uandaaji bora wa hesabu kwa kufuata viwango vya kimataifa (International Financial Reporting Standards – IFRS).
Tuzo hiyo ilipokelewa na Kamishna wa DCEA, Hussein Mbaga, kwa niaba ya Kamishna Jenerali, Aretas Lyimo, katika hafla iliyofanyika tarehe 29 Novemba 2024, kwenye Kituo cha Wahasibu cha Bunju, Dar es Salaam.
Kamishna Mbaga alibainisha kuwa ushindi huo ni matokeo ya juhudi kubwa za Mamlaka katika kuimarisha uwazi na uwajibikaji wa kifedha. “Tunamshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha taasisi zetu zinapatiwa rasilimali za kutosha, ambazo zimetumika kwa ufanisi kufanikisha majukumu yetu,” alisema.
Aidha, aliipongeza timu ya DCEA kwa kujituma na kufanikisha utekelezaji wa majukumu yao kwa viwango vya juu. “Ushindi huu ni wa timu nzima, ambao umejikita katika misingi imara ya uwajibikaji,” aliongeza.
Muhasibu Mkuu wa DCEA, Steven Galatia, alieleza kuwa mafanikio hayo yametokana na ushirikiano wa karibu na Hazina, ambapo wamehakikisha fedha zote zinatumika kwa misingi iliyoelekezwa. “Tumefuata maelekezo yote kutoka Hazina kwa umakini mkubwa, na hilo limekuwa chachu ya ushindi huu,” alisema Galatia.
Aidha, Galatia alitoa shukrani kwa waandishi wa habari kwa mchango wao wa kuhamasisha umma kuhusu juhudi za mamlaka hiyo katika kupambana na matumizi ya dawa za kulevya, ambazo ni hatari kwa afya ya jamii. “Tunategemea waandishi wa habari kama washirika wetu muhimu katika kampeni hizi,” alisisitiza.
Ushindi huu unakuja wakati ambapo DCEA inaendelea kupanua wigo wa operesheni zake za kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya nchini. Mafanikio haya yanaweka msingi mzuri kwa mamlaka hiyo kuimarisha zaidi utendaji wake na kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha jamii inalindwa dhidi ya janga la dawa za kulevya