Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeendesha mafunzo maalum kwa wafanyakazi wa benki za biashara jijini Dodoma, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kuondoa kwenye mzunguko noti za zamani. Zoezi hili linalotarajiwa kuanza rasmi tarehe 6 Januari 2025 na kumalizika tarehe 5 Aprili 2025, linalenga kuhakikisha uelewa wa kutosha kuhusu utekelezaji wake miongoni mwa wadau wa sekta ya benki.
Mafunzo hayo yaliongozwa na Meneja Uendeshaji wa BoT Tawi la Dodoma, Bw. Nolasco Maluli, ambapo washiriki walipata fursa ya kujifunza kwa vitendo namna ya kutambua alama za usalama zilizopo katika noti za zamani zitakazoondolewa. Pia walielekezwa hatua muhimu za kufanikisha mchakato huo kwa uwazi na ufanisi.
Kwa mujibu wa BoT, noti zitakazoondolewa kwenye mzunguko ni pamoja na shilingi 20, 200, 500, 1,000, 2,000, 5,000 na 10,000 kwa matoleo ya mwaka 1985 hadi 2003, pamoja na noti ya shilingi 500 ya mwaka 2010. Noti hizi hazitakuwa halali kama fedha kuanzia tarehe 6 Aprili 2025, ambapo benki zote zitapigwa marufuku kupokea, kubadilisha au kulipa malipo kwa kutumia noti hizo.
Wananchi walio na noti hizo watahitajika kuwasilisha fedha zao kwenye ofisi za Benki Kuu au benki za biashara ili kubadilishiwa thamani inayolingana na fedha walizonazo kabla ya ukomo wa matumizi.
Zoezi hili linalenga kuboresha mfumo wa fedha nchini kwa kuzingatia alama za usalama zinazozingatia viwango vya kisasa na kuhakikisha usalama wa noti zinazotumika katika mzunguko wa fedha.