MBUNGE wa Jimbo la Chaani, Juma Usonge Hamadi, akikata utepe kuashiria ufunguzi wa Madrasat Nuru-l-huda iloyopo Muharitani Kinyasini Wilaya ya Kaskazini ‘A’ Unguja. (PICHA NA MPIGA PICHA).
NA FAUZIA MUSSA
WAZAZI na walezi wametakiwa kushirikiana na walimu wa madrasa kuwalinda watoto wao na vitendo vya udhalilishaji ambavyo bado vinaonekana kuwepo nchini.
Mbunge wa Jimbo la Chaani, Juma Usonge Hamadi aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na walimu, wazazi na wanafunzi wa madrasat Nuru-l-huda wakati wa ufunguzi wa madrasa hiyo uiyoambatana na kusherehekea mazazi ya Mtume Muhammad S.A.W huko Muharitani Kinyasini Wilayani ya Kaskazini ‘A’ Unguja.
Alisema licha ya Serikali na wadau mbalimbali kukemea vitendo hivyo na adhabu kutolewa kwa watendaji lakini bado vinaonekana kujirejea siku hadi siku na kusema kuwa ipo haja kwa jamii kuimarisha ulinzi wa watoto ili kuepukana na vitendo hivyo.
“Kutoka na hali ya utandawazi na mporomoko wa maadili, ni vyema kashirikiana kuwajengea uwezo watoto wetu, wa kujua na kujiepusha na vitendo vya udhalilishaji na ukatili wa kijinsia unaoweza kutokea popote maisha yao hata katika madrasa.” Alisema Usonge
Usonge aliwasisitiza walimu na wazazi kuendelea kuwasimamia watoto kupata elimu zote mbili, na kuwataka wanafunzi hao kusoma kwa bidii na kuwa na nidhamu kwani ni mambo ya msingi katika kufikia ndoto zao za maisha.
Mbali na hayo aliwapongeza walimu wa madrasa hiyo kwa kuwa wastahmilivu kipindi chote walichokuwa na mazingira magumu ya kufundishia hadi kufanikiwa kupata jengo hilo litakaloondoa changamoto ya ufinyu wa vyumba vya madrasa iliyokuwepo hapo awali.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Madrasa hiyo Ustadh Ali Khamis Foum, alisema suala la udhalilishaji na ukatili wa kijinsia likemewa katika dini zote, hivyo ni vyema jamiii ikasimamia makatazo hayo ili kukomesha vitendo vya udhalilishaji nchini.
Alibainisha kuwa kupatikana kwa jengo hilo lenye vyumba vitatu vya kujifunzia, kutaondosha mrundikano wa wanafunzi wengi katika darasa moja, jambo ambalo alilitaja lingeweza kuhatarisha afya zao.
Vilevile alisema ongezeko la vyumba hivyo pia kutaondoa changamoto ya kuchanganya wanafunzi wa jinsia mbili katika chumba kimoja, jambo ambalo alilitaja lingechochea wanafunzi kudhalilishana wao kwa wao kama halikutatuliwa.
“ Kabla ya jengo hili baadhi ya wanafunzi walilazimika kusoma nje ya chumba kimoja kilichokuwepo, kupata vyumba hivi itasaidia wanafunzi wetu wote kusoma ndani” alisema mwalimu huyo
Hata hivyo aliwataka wazazi na walezi kuwa karibu na walimu kwani kukose mashirikiano kunazorotesha maendeleo ya elimu kwa wanafunzi.
Baadhi ya wazazi wa wanafunzi wa madrasa hiyo waliwaomba wadau na wahisani kuwasaidia kuongeza vyoo katika madrasa hiyo ili kulinda afya za wanafunzi.
“mwanzo madrasa hii ilikuwa na vyoo viwili na sasa ina vyoo vinne lakini bado havitoshelezi kutokana na wingi wa wanafunzi na walimu waliopo katika madrasa hii” walisema
Madarasa hiyo ilionzishwa mwaka 1995, ina wanafunzi 257 wakiwemo wanawake158 na wanaume 99, pamoja na walimu 7 Wanawake 4 na wanaume 3 ambapo katika hafla ya ufunguzi wa madrasa hiyo, mbunge Usonge alikabidhi kiasi cha shilingi laki mbili kwaajili ya vikalio na kuahidi kutoa vitabu, vijuzuu na misahau kwa wanafunzi hao.