Mhasibu Mkuu wa serikali CPA .Leonard Mkude akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na mkutano huo .
Mwenyekiti wa Umoja wa wahasibu wakuu wa Afrika, Malehlohonolo Mahase akizungumzia mkutano huo .
Mkurugenzi Mtendaji wa kituo cha AICC ,Christine  Mwakatobe akizungumzia mkutano huo  
………………… 
Happy Lazaro,Arusha .

Arusha .TANZANIA inatarajiwa kuwa mwenyeji wa mkutano Mkuu  wa pili wa Wahasibu wakuu wa serikali wa bara la Afrika(AAAG)  unaotarajiwa kufanyika desemba 2 hadi 5 katika ukumbi  wa mikutano wa Aicc mkoani Arusha .

Akizungumza  na waandishi wa habari mkoani Arusha kuhusiana na mkutano huo,Mhasibu Mkuu wa serikali CPA .Leonard Mkude amesema kuwa,mkutano huo unafanyika kwa mara ya pili tangu kuanzishwa kwake julai 5,2023 ambapo kwa  mara ya kwanza ulifanyika nchini Lesotho febuari 2024.
Amesema kuwa , Umoja wa Wahasibu Wakuu wa serikali Afrika ulizinduliwa rasmi Mombasa,Kenya julai 5 ,2023 baada ya Azimio la kufunga Umoja wa Wahasibu uliokuwepo  katika kanda mbalimbali, ambapo kwa sasa nchi 55 za umoja wa Afrika ni mwanachama wa Umoja huu. 
“Lengo la Mkutano wa kimataifa wa Wahasibu ni kujenga imani ya Umma katika mifumo ya usimamizi wa fedha za Umma kwa ukuaji  endelevu.”amesema .
Aidha ameongeza kuwa , inakadiriwa kuwa watu zaidi ya  2000  watashiriki  mkutano huo wakiwemo Wahasibu,Wakaguzi wa hesabu, Wataalamu wa masuala ya fedha, Tehama,Vihatarishi n.k ambapo walengwa hao ni wale walioajiriwa serikalini, makampuni binafsi pamoja na waliojiajiri. 
Ameongeza kuwa ,mkutano huo utawaleta  pamoja wahasibu wakuu wa serikali wa Afrika watakaofuatana na Wahasibu wakuu wa wizara,Taasisi za umma ,wahasibu wa ngazi tofauti  tofauti na wadau wengine ,kutoka nje ambao watakuja na fedha za kigeni ambazo watazitumia hapa Tanzania .
Amefafanua kuwa, wahasibu na wakaguzi wa hesabu watakaohudhuria watapata  fursa ya kusikiliza mada za masuala mbalimbali ya kitaaluma ,sambamba na kukutana na wahasibu wakuu wa serikali wa Afrika na kubadilishana mawazo na kupeana mawasiliano,kujua fursa zinazopatikana katika nchi za kiafrika. 
Aidha ametoa wito  kwa wahasibu ,wakaguzi wa hesabu na wadau wengine  wote hususani watanzania kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kuhudhuria mkutano huo mkubwa kwa njia ambazo zitatajwa huku kuwataka maafisa masuuli  wa wizara na taasisi zote kuwaruhusu wahasibu  na wakaguzi watakaoomba kuhudhuria mkutano huo.
Mwenyekiti wa Umoja wa wahasibu wakuu wa Afrika, Malehlohonolo Mahase,amesema kuwa,faida za mkutano huo ni pamoja na kuwa na Afrika yenye  mafanikio yenye msingi wa ukuaji jumuishi na maendeleo endelevu,bara jumuishi lililounganishwa kisiasa  kwa kuzingatia maadili ya Pan-Africanism na maono ya mwamko wa Afrika,pamoja na kuwa na Afrika yenye utawala bora, demokrasia, kuheshimu haki za binadamu ,haki na utawala wa sheria .
Amefafanua kuwa baada  ya mkutano huo wanatarajia  kuwa na Afrika yenye amani  na usalama na yenye utambulisho thabiti wa kitamaduni, urithi wa pamoja na maadili.
“Nchi ya Tanzania ina maswala mazuri ya uzalendo  na kupitia mkutano huu  tutaweza kujifunza maswala mazuri yanayofanywa na nchi ya Tanzania ikiwemo usimamizi mzuri wa fedha pamoja na kuja kuangalia fursa mbalimbali za uwekezaji.”amesema .
Mkurugenzi Mtendaji wa kituo cha AICC ,Christine  Mwakatobe amesema kuwa ,wamejipanga vyema kuhakikisha wageni wanapokuja waweze  kutoa huduma bora .
Aidha amemshukuru  Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutangaza nchi yetu  duniani kwani hiyo ni  kazi kubwa aliyoifanya   ya kutangaza  utalii kwani  wameona mikutano mingi na wawekezaji wanaendelea  kuja  .