Afisa Mwandamizi Bodi ya Bima ya Amana katika Benki hiyo Bi. Joyce Shala akizungumza kwenye Maonesho ya Biashara ya 47 ya Kimataifa yanayoendelea kwenye viwanja vya Sàbasaba Barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.
………………………..
BENKI Kuu Ya Tanzania imesema kuwa zaidi ya asilimia 98 ya wateja waliopo katika Benki na Taasisi za fedha nchini wana kinga ya bima ya amana.
Pia, wateja wote wenye viwango vya fedha kuanzia shilingi millioni moja(1) mpaka milioni 7,500,000 wanapata pesa yao pale benki au taasisi ya fedha inapofilisika.
Hayo yamebainishwa na Afisa Mwandamizi Bodi ya Bima ya Amana katika Benki hiyo Bi. Joyce Shala alipozungumza na waandishi wa habari kwenye Maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba), yanayofanyika katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere Jijini Dar es salaam namna Bodi hiyo inavyotekeleza majukumu yake.
Amesema kuwa kama zilivyo Bodi za Bima za Amana nyingine ulimwenguni, Benki kuu ya Tanzania (BoT), iliteua Bodi ya Bima ya Amana nchini, kwa lengo la kuwalinda wenye wateja wenye amana kutokana na athari ya kupoteza amana zao pale kunapotokea changamoto inayopelekea Benki au Taasisi ya fedha kufilisika.
“Bodi yetu ya Bima ya amana ina jukumu la kusimamia mfuko wa Bima ya Amana (Deposit Insurance Fund – DIF), ili kuwepo na Bima ya Amana inayotoa kinga kwa wenye Amana katika Benki au Taasisi ya fedha inapofilisika, au kuwekwa katika ufilisi.
“Kwa sasa Bodi yetu inatoa kiwango kipya cha fidia ambapo kuanzia mwezi Februari 2023, ikitokea Benki au Taasisi ya fedha imeanguka au kufungwa, watapata kuanzia Shilingi moja (1) mpaka milioni saba na laki Tano, (7,500,000)”
Alisema kuwa Tanzania ni mahali salama kufanya biashara na uwekezaji kwani fedha zao ziko salama chini ya usimamizi wa Benki Kuu yenye jukumu la kusimamia sekta zote za fedha.
“Tunawahakikishia wafanyabiashara na wawekezaji kuwa Tanzania ni mahali sahihi pa kufanyia Biashara na Uwekezaji kwani fedha za watanzania ziko salama chini ya usimamizi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), yenye jukumu la kusimamia sekta zote za fedha nchini, ikiwemo Bodi ya Bima ya Amana (DIB) kwaajili ya kukinga Amana za wenye Aamana zao pale ambapo kwa bahati mbaya Benki imefungwa” ameeleza Bi. shala.
Ameongeza kusema kuwa Bodi hiyo pia ina jukumu la kusimamia ufilisi wa Mabenki au Taasisi ya fedha pale ambapo Bodi ya Bima ya Amana imeteuliwa na Benki Kuu ya Tanzania kufanya kazi hiyo.
Kwa sasa Bodi ya Bima ya Amana inaendelea na ufilisi wa zilizokuwa Greenland Bank (T) Limited, Delphi’s Bank (T) Limited, FBME Bank Limited, Mbinga Community Bank Plc, EFATHA Bank Limited, Njombe Community Bank limited, Kagera Famers’ Cooperative Bank limited, na Meru Community Bank Limited

Afisa Mwandamizi Bodi ya Bima ya Amana katika Benki hiyo Bi. Joyce Shala akizungumza kwenye Maonesho ya Biashara ya 47 ya Kimataifa yanayoendelea kwenye viwanja vya Sàbasaba Barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.

