*********************
Na Mwandishi wetu,Dar Es Salaam
Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko ameongoza kikao kati ya Wizara na Kampuni za dmg events  na Ocean Business Partners Tanzania  ambazo zinashirikiana kuandaa Jukwaa la Kimataifa la Uwekezaji katika Sekta ya Madini Tanzania kwa mwaka 2023  kwa kushirikiana na Wizara.
Mkutano huo wa Kimataifa uliokuwa ukifanyika mwezi Februari ya kila mwaka, mwaka huu utafanyika tarehe 25-26 Oktoba, 2023 jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika  Februari 18, 2023 jijini Dar es Salaam,  Waziri Dkt. Biteko amewaeleza wawakilishi wa kampuni hizo kuwa, Wizara inatarajia kupata matokeo makubwa  kutokana na kuitangaza sekta ya Madini kimataifa ili kuhamasisha uwekezaji kutokana na nchi  ya Tanzania kubarikiwa kuwa na madini mengi yakiwemo ya kimkakati ambayo yanahitajika duniani kwa sasa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Ocean Business Partners Tanzania Balozi wa Heshima Brazil- Zanzibar Abdulsamad Abdulrahmim ameipongeza wizara ya madini kwa kukubali kushirikiana na kampuni  hizo binafsi kuandaa mkutano huo .
Amesema mbali ya mkutano huo kutarajiwa kuitangaza Sekta ya Madini, pia, itawezesha kuhamasisha uwekezaji na kuzalisha ajira kutokana na shughuli mbalimbali zitakazofanyika  kipindi cha mkutano huo.