Na Tiganya Vincent-Mahakama ya Tanzania
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi katika hafla za uzinduzi wa majengo 18 ya Mahakama ya Wilaya kesho tarehe 25 Novemba, 2022 katika jengo jipya la Mahakama ya Wilaya ya Busega, mkoani Simiyu.
Uzinduzi huo ni mwendelezo wa uzinduzi wa miradi ya majengo ya mahakama inayoendelea kuzinduziwa nchini ambapo mpango wa uongozi wa mahakakam ni kuzindua jumla ya majengo ya mahakama 26 hadi Disemba 2022.
Majengo 18 ya mahakama za wilaya yatakayozinduliwa kwa pamoja siku hiyo yamejengwa kwa ufadhili wa mkopo yenye nafuu kutoka Benki ya Dunia kwa Serikali ya Tanzania kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya Mahakama.
Katika miradi hiyo 18, miradi 15 ni ya mahakama mpya za wilaya ambazo hazikuwa na huduma za Mahakama ya wilaya na 3 ni mahakama za wilaya zilizokuwa na majengo chakavu.
Mahakama za Wilaya zinatarajiwa kuzindiliwa siku hiyo ni Nyang’ale, Mbongwe , Kaliua, Uvinza, Kakonko, Buhigwe, Kyerwa, Misenyi, Kilombero, Mvomero, Gairo, Songwe, Butiama, Rorya, Tanganyika, Itilima, Busega na Mkinga.
Ujenzi wa miradi hii mbayo ipo katika mikoa tofauti hapa nchini umezingatia mahitaji ya kisasa kwa wadau wa mnyororo wa utoaji haki ambapo zipo ofisi za Mawakili, Maafisa Magereza, Ustawi wa Jamii. Watu wenye mahitaji maalum na watoto wamewekewa vyumba vya kutumia wakiwa mahakamani hapo.
Kuzinduliwa kwa majengo hayo katika Wilaya hizo 18 kutaongeza ufanisi na utoaji huduma kwa wananchi kwani majengo haya yana mzingira rafiki ya utoaji wa huduma kwa wananchi kwa kutumia mfumo ya kitekinolojia. Huu ni utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Mahakama wa Miaka mitano (5) wa 2020/21-2024/25 nguzo ya upatikanaji wa haki kwa wakati kupitia uboreshaji wa miundombinu ya majengo na kusogeza huduma za haki karibu na wananchi.
Halfa ya uzinduzi inatarajiwa kuhudhuriwa na Viongozi Waandamizi mbalimbali wa Mahakama, Serikali na Bunge wakiwemo Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani, Majaji wa Mahakama Kuu, Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Dunia, Msajili Mkuu wa Mahakama Mhe. Wilbert Chuma, Waziri wa Fedha na Uchumi, Dkt. Mwigulu Nchemba, Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Damas Ndumaro, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Dkt. Yahya Nawanda na Wabunge.
Wananchi wa Mkoa wa Simiyu, Wilaya ya Busega na Wilaya za jirani wanaombwa kujitokeza katika Viwanja vya Mahakama ya Wilaya ya Busega kushuhudia uzinduzi huo ambao ni ishara ya kuwepo mabadiliko makubwa ya maboresho ya utoaji huduma za Mahakama nchini.
Halikadhalika wananchi wa maeneo mbalimbali nchini wanaweza kufuatilia tukio hilo mubashara kupitia Televisheni ya Taifa (TBC).