MKURUGENZI Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD) Mavere Ali Tukai,akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Utekelezaji wa Shughuli mbalimbali za Taasisi hiyo na mwelekeo wa utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2022/2023 leo Oktoba 17,2022 jijini Dodoma.
WAANDISHI wa Habari wakimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD) Mavere Ali Tukai,wakati akitoa taarifa kuhusu Utekelezaji wa Shughuli mbalimbali za Taasisi hiyo na mwelekeo wa utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2022/2023 leo Oktoba 17,2022 jijini Dodoma.
MKURUGENZI wa Idara ya Habari – MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa,akielezea nia nje ya Serikali kuhusu Sheri ya Bima kwa Wote mara baada ya Bohari ya Dawa (MSD) kutoa taarifa ya Utekelezaji wa Shughuli mbalimbali za Taasisi hiyo na mwelekeo wa utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2022/2023 leo Oktoba 17,2022 jijini Dodoma.
……………………………………………
Na Alex Sonna-DODOMA
MKURUGENZI Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD) Mavere Ali Tukai,amebainisha vipaumbe vya MSD kwa mwaka 2022-2023 ambavyo ni kuimarisha upatikanaji wa dawa hadi kufikia asilimia 90 ya mahitaji kwa kuingia mkataba wa muda mrefu na wazalishaji wa bidhaa za afya.
Vipaumbele hivyo amevitaja leo Oktoba 17,2022 jijini Dodoma wakati akitoa taarifa kuhusu Utekelezaji wa Shughuli mbalimbali za taasisi hiyo na mwelekeo wa utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
Bw.Tukai ametaja kipaumbele kingine ni kufanya mabadiliko ya kimuundo na kimfumo ambapo yapo katika hatua za mwisho za kuhakikisha inapata menejimenti mpya.
“Aidha, inaendelea na mabadiliko ya ndani ya Taasisi yanayolenga kuimarisha utendaji na upatikanaji wa bidhaa za afya.
AVipaumbele vingine ni kuongeza kasi ya ununuzi kwa kuzingatia kanuni, taratibu na sheria.
Amesema wanaendelea kushirikiana na Mamlaka ya Serikali Mtandao kuhakikisha taratibu zote za ndani zinawekwa kwenye mfumo ili kuongeza ufanisi katika eneo la manunuzi.
“MSD inafanya mapitio ya maboresho ya mfumo mzima wa mnyororo wa ugavi kwa kuhusisha wadau mbalimbali kwani lengo la kuhakikisha uendeshaji wa taasisi unaendana na mahitaji ya vituo vya afya na wadau wengine.
“Tutaendelea na utekelezaji wa mchakato wa kumpata mbia wa ujenzi wa viwanda vya bidhaa za afya vya ndani kwa kutumia PPP
“Tutaendelea na juhudi za kuboresha miundombinu yetu na kusogeza huduma karibu na wananchi kwa kufanya ujenzi wa maghala ya kisasa katika mikoa ya Kagera na Ruvuma.
“Kuongeza ushirikiano na wadau wetu wakuu wakiwemo wafadhili, washitiri, wateja pamoja na sekta nyingine ambazo tunafanya nao kazi,”amesema Mkurugenzi huyo
Amesema wanashirikiana na sekta zingine kuhakikisha wananyanyua wazalishaji wa ndani ya nchi hasa kwenye kuwakaribisha wawekezaji wenye nia ya dhati ya kuwekeza kwenye uzalishaji wa bidhaa za afya
Aidha amesema MSD ina majukumu manne ya uzalishaji, ununuzi, utunzaji na usambazaji wa bidhaa za afya kwenye vituo vya umma vya kutolea huduma za afya na vituo binafsi vilivyoidhinishwa na Wizara ya Afya
Amesema katika mwaka wa fedha 2021/22, Serikali ilitoa Shilingi bilioni 134.9 kwa ajili ya ununuzi wa bidhaa za afya.
“MSD inaendelea na zoezi la usambazaji wa bidhaa za afya kwenye vituo vyote vya afya vya Serikali 7,153 kupitia kanda zake 10 zilizowekwa kimkakati.MSD ina maduka ya jamii sita yaliyopo katika mikoa ya Katavi, Arusha, Lindi, Mbeya, Geita na Dar es Salaam ili kusaidia kusogeza huduma kwa wananchi,”amesema.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Habari – MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema Serikali ina Sera inayotaka kuwepo kwa dawa, vifaa na vifaa tiba vitendanishi vya kutosha, vyenye ubora, na Watanzania wavipate kwa bei wanayoweza kumudu.
“Mpaka sasa, kwenye hospitali zetu za Mikoa, Kanda, Rufaa na kitaifa upatikanaji wa dawa uko asilimia 80 kwa sababu wanapata dawa kutoka MSD na zingine wanazipata kutoka kwenye maeneo mengine,”amesema.
Aidha Msigwa amezumgumzia Sheria ya Bima ya afya kwa wote kuwa ni nia njema ya serikali kuhakikisha kila mtanzania anapata matibabu ya aina yeyote kwa gharama yeyote na kuondokana na adha wanayokutana nayo pindi wanapokosa huduma kutokana na kukosa fedha.
“Niwahakikishie kuwa nia ya serikali ni njema sana juu ya wananchi wake epukaneni na wapotoshaji ambao wanapotosha taarifa hizi juu ya hii sheria ya bima ya afya kwa wote hii ni namna nzuri ya kuhakikisha kila mtanzania anapata matibabu bila changamoto yeyote,”Amesema Msigwa
Bohari ya Dawa ni Taasisi ya serikali iliyopo chini ya Wizara ya afya, iliyoundwa kwa sheria ya Bunge namba 13 ya mwaka 1993 ili kununua,kutunza na kusambaza bidhaa za afya ila kutokana na mabadiliko ya sheria ya Bohari ya Dawa ,sura ya 70 iliyoidhinishwa mwezi oktoba 2021 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani imeiwezesha MSD kuanza kuzalisha bidhaa za afya kama jukumu lake la nyongeza,kwenye majukumu yake ya msingi.