Katibu Mkuu,Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu Prof. Jamal Adam Katundu (katikati), pamoja na Abu Sayed Mkurugenzi wa Taasisi ya ASA Microfinance Tanzania Limited (kushoto), wakimkabidhi Mwenyekiti wa Shirika la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu Mkoa Wa Dodoma Ommary Lubuva (kulia) kiti mwendo (wheelchair) wakati wa hafla ya makabidhiano ya vifaa saidizi kwa watu wenye ulemavu iliyofanyika katika ofisi hiyo mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma, Oktoba 6, 2022.
Katibu Mkuu,Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu Prof. Jamal Adam Katundu (kulia) akikabidhi mafuta maalumu kwa ajili ya watu wenye ualbino kwa Mwenyekiti wa Shirika la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu Mkoa Wa Dodoma Omary Lubuva (katikati) wakati wa hafla fupi ya makabidhiano ya vifaa saidizi kwa watu wenye ulemavu iliyofanyika jijini Dodoma.
Katibu Mkuu,Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu Prof. Jamal Katundu (katikati) akiwa pamoja na viongozi wengine wakimkabidhi kiti mwendo (wheelchair) Bi. Sofia Muhando wakati wa hafla hiyo.
…………………………………….
Na Mwandishi Wetu-DODOMA
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye ulemavu Pro. Jamal Katundu,ameipongeza Taasisi ya ASA microfinance kwa kukabidhi vifaa vya thamani ya sh.milioni 13.5 kwa watu wenye ulemavu.
Akizungumza leo Oktoba 6,2022 jijini Dodoma mara baada ya kupokea vifaa hivyo Prof.Katundu ameipongeza taasisi hiyo kwa kuunga juhudi za Rais Samia kwa kuendelea kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili watu wenye ulemavu nchini.
Amesema vifaa vilivyokabidhiwa ni viti mwendo pisi 35, mafuta maalumu kwa ajili ya watu wenye ualbino 35 na fimbo maalumu kwa watu wenye matatizo ya kuona 35.
“ASA mmekuwa mkitoa misaada mbalimbali kwa ajili ya watu wenye ulemavu na tumekuwa tukitumia nafasi hii kuwaomba wadau wengine kuiga mfano wenu huku Mkiendelea kushirikiana na serikali”amesema Prof.Katundu
Hata hivyo amesema kuwa serikali inaendelea kuhamasisha taasisi nyingine kutoa msaada kwa kuwasaidia watu wenye mahitaji maalumu ili kuimarisha maendeleo yao, ustawi na taifa kwa ujumla.
”Sisi kama Serikali tunaendelea kuhamasisha taasisi mbalimbali na wadau kujitokeza kwa wingi katika kutoa misaada kwa watu wenye mahitaji maalumu ili kutatua changamoto zinazowakabili”amesema
Awali Mwanasheria wa Taasisi ya ASA microfinance Zephania Paul amesema vifaa vilivyotolewa na asasi hiyo vinathamani ya Tsh. Milioni 13.5 huku akisisitiza kuwa lengo ni kuona umuhimu wa kuishi na watu wenye mahitaji maalumu kwa kichache kinachopatikana.
“Taasisi yetu ya ASA imekuwa ikifanya hivy mara kwa mara kwa lengo la kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Serikali katika kuhakikisha anawaboreshea maisha Watu wenye Ulemavu nchini,”amesema
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye ulemavu Mkoa wa Dodoma, Omary Lubuva,ameishukuru taasisi hiyo kwa kutoa msaada huo ambao utawawezesha watu wenye ulemavu kujimudu na kushiriki kwenye shughuli mbalimbali.
“Sisi Watu wenye Ulemavu tunatambua na kuthamini jitihada na juhudu zinazofanywa na serikali yetu inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia katika kutatua changamoto zetu, tunaomba taasisi na asasi nyingine waweze kuona haya ambayo yanafanywa na baadhi ya wenzao ili na wao waone wanawezaje kushiriki katika kusaidia kuboresha masha yetu,” amesema
Naye, Bi. Sophia Mhando (mwenye ulemavu wa Miguu) amesema hajawahi kufikiri kuwa ipo siku atapata kiti mwendo kwa kuwa amekuwa akihangaika kutembea na kuomba omba hivyo kupata kiti mwendo hicho kitamwezesha kujishughulisha na shughuli za ujasiriamali.