Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt.Allan Kijazi akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni jijini Dar es Salaam
*********************
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeongeza siku za kusikiliza malalamiko ya migogoro ya Ardhi katika mkoa wa Dodoma baada ya siku tano za mwanzo kumalizika iikiwa kuna ongezeko kubwa la wananchi ambao hawajafikiwa.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt.Allan Kijazi amesema zoezi hilo limeongezewa siku tatu kwa Dodoma hii ni kutokana na malalamiko mengi na wananchi baadhi bado hawajasikilizwa.
Aidha,amesema pia wameona kwamba kuna haja ya wataalamu wao kabla ya kutoa mrejesho kwa badhi ya malalamiko wapate muda wa kufanya uchambuzi wa malalamiko ambayo yametolewa yafanyiwe uchambuzi.
“Hii itatusaidia kuweza kutatua migogoro kwa njia ya haki kwa kila mmoja bila ya kuwa na upendeleo wa aina yeyote na baada ya kumaliza maeneo ya Dodoma tunaendelea na zoezi katika mikoa mingine” amesema Kijazi.
Aidha, kwa upande wa upande wa Dar es salaam walipokea malalamiko 386 uchambuzi wa kina ulifanyika baadhi ya malalamiko yalishatolewa uamuzi na mengine yanaendelea kuchambuliwa katika nyaraka mbalimbali katika kumbukumbu zao ili kujiridhisha kabla ya kutoa maamuzi.
“Kwa wale wananchi ambao bado hawajapata mrejesho wasifikirie kwamba malalamiko yao hayakufanyiwa kazi yapo maeneo ambayo tulilazimika kukutanisha watu kama yanahusu pande mbili au tatu tukutanishe ili kuweza kusikiliza hoja ili tuweze kutoa maamuzi sahihi” amesema Kijazi.