Mkurugenzi Mkazi wa CARE International Bi.Prudence Masako akizungumza kwenye kikao kazi cha tathimini ya miradi TAJIRIKA NA KILIMO (TnK) na UJANA NI UCHUMI IMARA (UCHUMI) kilichofanyika April 22, 2022Mjini Morogoro.
Baadhi ya wadau wa kilimo na mifugo walioshiriki katika kikao hicho.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Tixon Nzunda akizungumza kwenye kikao kazi cha tathimini ya miradi TAJIRIKA NA KILIMO (TnK) na UJANA NI UCHUMI IMARA (UCHUMI) kilichofanyika April 22, 2022Mjini Morogoro.
……………………………………………….
NA FARIDA MANGUBE, MOROGORO.
CARE International Tanzania kupitia miradi yake ya TAJIRIKA NA KILIMO {TnK} na UJANA NI UCHUMI IMARA (UCHUMI) imetoa mafunzo kwa wanawake na vijana elfu mbili na miambili ishirini (2,220) ili waweze kujikomboa kiuchumi kupitia kilimo na ufugaji.
Mradi wa TAJIRIKA NA KILIMO (TnK) na UJANA NI UCHUMI IMARA (UCHUMI) umetekelezwa na CARE International Tanzania kwa ubia wa VETA na SAGCOT center Ltd. imekuwa na mnaufaa makubwa kwa wananchi hususani wale walioko katika vikundi vya kuweka na kukopa ambapo kundi kubwa la wanufaika hao ni wanawake na vijana.
Akizungumza kwenye kikao kazi cha tathimini ya miradi hiyo Mkurugenzi Mkazi wa CARE International Bi.Prudence Masako alisema CARE wanalenga kuwafikia watu milioni miambili lengo likiwa ni kupunguza umasikini kwa watanzania na kuleta haki hadi kufikia mwaka 2030
Alisema CARE imekuwa ikifanya kazi kubwa katika kuangalia namna gani jamii inaweza kutumia rasilimali zilizopo ili kujikwamua kiuchumi hususani kwa wanawake ambao wengi wao wamekuwa wakishindwa kujitetea na kukosa haki zao za msingi .
Kwa upande wake Meneja msimamizi wa miradi kutoka CARE Bwana.Samwel Chambi alisema kuwa miradi hiyo ya TAJIRIKA NA UCHUMI imekuwa ikihamasisha watu kujiunga katika vikundi na kujengewa uwezo hususani katika kilimo biashara na uchumi hasa kwa wanawake na vijana .
Aidha Chambi alibainisha kuwa mradi wa TAJIRIKA NA UCHUMI imekuwa fursa kwani imewapatia wanawake zaidi ya 3000 mafunzo ya ujuzi na vijana 15,000 mafunzo ya ujasiriamali , stadi za maisha , jinsia na usawa.
Hata hivyo imeelezwa kuwa fursa hizi zimetumika vyema kuchangia kupunguza tatizo la umasikini kwa vijana kwakuwa walengwa wamewezeshwa kuanzisha kilimo biashara na wengine ufugaji ili kujikwamua kiuchumni.
Akifungua kikao kazi hicho Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Tixon Nzunda ameviagiza vyuo vya ufundi stadi nchini VETA kuanza kutekeleza mara moja miataala ya kilimo biashara na uchumi , ambayo tayari imekamilika lengo likiwa ni kuongeza ujasiliamali , kipato na kuimarisha uchumi wa wananchi na Taifa kwa ujumla.
Alisema taasisi zote zinazotoa mafunzo zihakikishe zinatoa elimu ya mifugo na kilimo biashara ili vijana waweze kupata ujuzi na maarifa ya kilimo na ufugaji bora.
Hata hivyo alizitaka taasisi za mafunzo ikiwemo VETA, MATI NA LITA na sekta binafsi kuhakikisha kila mmoja kwa nafasi yake anatoa ushirikiano wa kutosha ili matokeo ya kazi zilizofanyika na miradi ya kilimo na uchumi zinaendelea kuwanufaisha wanajamii hata wale ambao hawakufikiwa moja kwa moja na miradi ya Tnk na UCHUMI.
Kikao hicho kilichofanyika mkoani Morogoro kimehudhuliwa na wadau mbalimbali wa kilimo na mifugo, wakurugenzi na wataalamu wa kilimo na mifugo kutoka Halmashauri zote ambazo miradi imetekelezwa pamoja na wanufaika wa miradi hiyo.