Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Mhandisi Juma Kijavara akiwaelezea wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Hesabu za Serikali (PAC) namna ya Mradi wa DMGP unavyotekelezwa bandarini hapo.
Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Bandari ya Tanzania (TPA), Eric Hamissi akiwaelezea wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Hesabu za Serikali (PAC) namna ya Mradi wa DMGP unavyotekelezwa bandarini hapo.
Naibu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) Mhandisi Karim Mataka, akiwaelezea wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Hesabu za Serikali (PAC) namna ya Mradi wa DMGP unavyotekelezwa bandarini hapo.
Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Hesabu za Serikali (PAC), wakiangalia miundombinu ambayo imeboreshwa katika Bandari ya Dar es Salaam kupitia Mradi wa DMGP.
…………………………………………………………….
Na Mwandishi Wetu
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), imesema uwekezaji wa zaidi ya Sh.trilioni 1 uliofanywa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), kwenye Bandari ya Dar es Salaam umeonesha tija na mafanikio makubwa.
Hayo yamesemwa na Makamu Mwenyekiti wa PAC, Japhet Hasunga wakati wa ziara ya kamati hiyo ilipotembelea bandari ya Dar es Salaam na kuona uwekezaji uliofanywa hadi sasa.
Hasunga amesema taarifa waliyopewa inaonesha ufanisi wa Bandari umeongezeka hali ambayo inachangia kuongeza mapato.
“Tumezungumza na menejimenti ya TPA na kutembelea maeneo ya uwekezaji kimsingi tumeridhishwa na maboresho yanayofanyika, tunawataka waongeze kasi ya usimamizi,” amesema.
Makamu Mwenyekiti huyo amesema uwekezaji wa takribani Sh.trilioni 1 umekuwa na tija katika baadhi ya maeneo ambapo matarajio yao ni kuona faida kubwa baada ya maboresho kukamilika.
Hasunga amesema kupitia uwekezaji huo Tanzania imeweza kupokea meli kubwa ambazo zinaingiza shehena nyingi za mzigo hivyo kuongeza mapato ya nchi.
Amesema ufanisi umeongezeka kwenye upakuaji wa shehena za mizigo kutoka siku 10 hadi siku tatu jambo ambalo ni la kupongezwa.
“Bandari ni taasisi nyeti kwenye kukusanya mapato, hivyo tunaomba Serikali kuongeza kasi ya uboreshaji Bandari ya Dar es Salaam ili kuongeza mapato na kukuza uchumi,” amesema.
Makamu Mwenyekiti ameipongeza TPA kwa hatua mbalimbali zinazochukuliwa kuboresha utendaji na ufanisi wa TPA.
Mwenyekiti huyo amesema kamati imeridhishwa na matumizi ya mifumo ya kisasa kwenye kuhudumia wateja jambo ambalo linaokoa muda na kuepusha upotevu wa mapato ya Serikali
Hasunga amesema pamoja na juhudi zinazofanyika kuongeza wigo wa masoko Kamati imeilekeza Menejimenti ya TPA kutafuta masoko zaidi katika nchi zote jirani kama DR Congo, Zambia, Burundi, Rwanda, Uganda na Sudani Kusini, hali ambayo itawezesha kuongeza mapato ya Mamlaka na nchi kwa ujumla.
Aidha, Hasunga ameitaka TPA kuhakikisha mitambo mipya inawasili kwa wakati ili kuongeza uzalishajiu.
“Pia tumewashauri washirikiane na wenzao wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kuhakikisha huduma hizo zinakuwepo mradi ukikamilika,” amesema.
Mwenyekiti wa Bodi ya TPA Balozi Ernest Mangu amesema mamlaka imechukua maelekezo ya kamati kuhakikisha bandari zote zinakuwa na tija.
“Sisi tunajipanga kuhakikisha maboresho makubwa yanafanyika kwenye bandari zetu kwa kila mtu kujituma,” amesema.
Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Eric Hamissi amesema mamlaka inaendelea kutekeleza mradi hatua kwa hatua ili ukamilike kwa wakati.
Hamissi amesema mradi wa kuboresha Bandari ya Dar es Salaam ( DMGP) umeanza 2017 na unatakiwa kukamilika 2024, kama ulivyopangwa.
“Mradi huu unatakiwa kukamilika 2024 na hili ndilo tunalipigania ili kuepusha gharama kuongezeka,” amesema.
Hamissi amesema mradi wa DMGP unahusu kuchimba kuboresha Gati Na. 1-7 kwa kuongeza kina cha gati kufikia mita 14.5, kujenga Gati jipya la magari (RO-RO), na kuchimba kina cha lango Bandari la kuingilia meli kufikia mita 15.5 na kuongeza mzunguko wa kugeuzia meli, kazi inayoendelea.
Hamissi amesema katika Awamu nyingine ya Mradi TPA itatoa mafunzo kwa wafanyakazi wake ili kuwajengea uwezo.