Wanawake kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma wakiongozwa na Mwenyekiti wa Wanawake Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Amina Tindwa wa kwanza kushoto alibeba katoni ya sabuni wakiwa katika kituo cha kulelea watoto yatima cha Upendo kilichopo Sanangula Manispaa ya Songea wakitoa msada wenye thamani ya shilingi 425,000.

************************

WANAWAKE kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma wametoa msaada wa vifaa mbalimbali vyenye thamani ya shilingi 425,000 katika kituo cha kulelea watoto yatima  cha Upendo kilichopo mjini Songea.

Wanawake hao wametoa msaada huo ikiwa ni sehemu ya kuelekea siku ya wanwake Duniani ambayo kilele chake ni Machi 8 mwaka huu.

Akizungumza kabla ya kutoa msaada huo, Mwenyekiti wa Wanawake katika Ofisi hiyo Amina Tindwa amesema katika kuadhimisha wiki ya Wanawake Duniani wanatembelea vituo mbalimbali vya watu wenye uhitaji na wanaoishi kwenye mazingira magumuj kwa kuwa mwanamke ni mlezi katika familia.

“Msaada ambao tumeutoa katika  kituo hiki ni mbolea pamoja na bidhaa zingine  ambazo zimegharimu kiasi cha shilingi  425,000’’,alisisitiza.

Kwa upande wake Mkuu wa Kituo hicho Sista Benigina Kapinga amesema kituo hicho kina watoto 24 ambao mmoja yupo chuo na wengine  wanasoma  shule za Sekondari na  shule  za msingi.

 Sista Kapinga amewashukuru wanawake hao kwa moyo wa upendo ,hata hivyo ameiomba serikali  kusajiliwa kituo hicho ili kitambulike na waweze kupata misaada mbalimbali.

Naye Afisa Maendeleo ya  Jamii Mkoa wa Ruvuma Exerveria Mlimila amemshauri  Mkuu wa kituo hicho kufanya jitihada ya kusajili  kituo hicho ili kitambulike na kuweza  kupata misaada mara kwa mara  hivyo  kukidhi mahitaji ya watoto hao.

Imeandaliwa na Aneth Ndonde

Kutoka Ofisi ya Habari ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma

Marchi 3,2022.