
***********************
NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) wamefunga Kampeni yao ya KAMILIKA 2022 ambayo ilikua inafanyika katika viwanja vya Mlimani City Jijini Dar es Salaam kwa kutoa hudma mbalimbali zikiwemo kusajiliwa majina ya biashara, kutoa leseni za biashara pamoja na utoaji wa elimu.
Akizungumza na waandishi wa habari katika viwanja hivyo, Afisa Usajili BRELA, Bi.Lucy Mbaga amesema katika kipindi chote hicho wakiwa wanatoa huduma muitikio wa watu wananchi umekuwa mkubwa kwani mpaka sasa wameshawahudumia wananchi takribani 2000.
Amesema wapo hapo toka Januari 26 mwaka huu ambapo kampeni hiyo ilikuwa ya siku nne lakini kutokana na uwepo wa wananchi wengi wakihitaji huduma imewalazimu kuongeza siku tatu ili kuweza kuwapa huduma wananchi.
Aidha Bi.Lucy amesema wapo kwenye mkakati wa kuwafika wananchi waliopo kwenye mikoa mbalimbali hapa nchi ili na wao waweze kupata huduma kwa urahisi na uhakika.
Bi.Lucy amesema changamoto kubwa wanayokutana nayo kutoka kwa wateja ni pamoja na wananchi wengi wao hawafahamu teknolojia ya online hivyo wamekuwa wakiwaelewesha ili waweze kupata huduma nzuri na kwa haraka zaidi.
