Waziri wa Kilimo Mhe. Prof Adolf Mkenda,akizungumza na waandishi wa habari leo November 28,2021 jijini Dodoma kuhusu mafanikio ya Sekta ya Kilimo katika kipindi cha miaka 60, ya uhuru wa Tanganyika.
Baadhi ya Waandishi wa Habari wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Kilimo Mhe. Prof Adolf Mkenda (hayupo pichani) wakati akiwasilisha mafanikio ya Sekta ya Kilimo katika kipindi cha miaka 60, ya uhuru wa Tanganyika.
Waziri wa Kilimo Mhe. Prof Adolf Mkenda ,akijibu maswali mbalimbali yaliyoulizwa na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo November 28,2021 jijini Dodoma wakati akizungumzia mafanikio ya Sekta ya Kilimo katika kipindi cha miaka 60, ya uhuru wa Tanganyika.
……………………………………………………
Na.Alex Sonna,Dodoma
WIZARA ya Kilimo imetaja mafanikio ambayo imeyapata katika kipindi cha miaka 60 ya uhuru wa Tanzania Bara pamoja na kujikita katika utafiti lengo likiwa ni kumsaidia mkulima aweze kulima kwa tija.
Hayo yamesemwa leo Novemba 28,2021 jijini Dodoma na Waziri wa Kilimo Prof.Adolf Mkenda wakati akizungumzia mafanikio ya Sekta ya Kilimo katika kipindi cha miaka 60, ya uhuru wa Tanganyika.
Waziri Mkenda amesema mwelekeo wa Wizara hiyo ni kujikita zaidi katika utafiti.
“Utafiti ndio kipaumbele chetu lengo tupate mbegu bora ambazo zitawasaidia wakulima,”amesema.
Amesema ili kufanya vizuri katika kilimo mikakati yao ni kujikita katika utafiti kwa kuwasaidia watafiti waweze kufanya tafiti mbalimbali ambazo zitasaidia na kuleta tija katika sekta ya kilimo.
Amesema Wizara ya Kilimo imeongeza vituo vya utafiti kutoka vitano mpaka 17 lengo likiwa ni kuweza kupata mbegu bora ambazo zitawasaidia wakulima kulima kilimo chenye tija.
UHABA WA MAFUTA
Waziri Mkenda amesema Serikali imeweka mikakati mbalimbali ikiwemo kuanzisha kampeni ya kulima zao la alizeti pamoja na kilimo cha Mchikichi lengo likiwa ni kupata mafuta.
“Kwenye michikichi itachukua muda mrefu kidogo na tutaenda mbali zaidi kuhakikisha tunajitosheleza katika kila kitu ikiwemo kwenda mpaka katika soya,”amesema.
TIJA NDOGO
Waziri Mkenda amesema changamoto kubwa ambayo wanakutana nayo ni tija ndogo ambapo amedai wakiingia katika soko lazima tija iwe kubwa ili waweze kushindana katika kuuza.
“Mchango wa kilimo kwenye uchumi ni asilimia 26 na mazao ni asilimia 15 na nimesema Nchi ikiendelea mchangao unapungua lakini mchango wa kilimo katika ajira lazima upungue zaidi,sisi bado watu ambao wanategemea kilimo moja kwa moja ni asilimia 58 maana yake ni tija ndogo,”amesema
Amesema ilikotoka Nchi asilimia 90 ya wananchi walikuwa wanategemea kilimo lakini sasa hivi asilimia 58 ndio wanaotegemea kilima kutokana na sababu mbalimbali.
UGANI NA KUWAFIKIA WAKULIMA WENGI
Aidha,Waziri Mkenda amesema kwa sasa watanzania wameongezeka tofauti na miaka ya nyuma hivyo wanahitajika maafisa ugani wengi ambao watawafikia wakulima kiurahisi.
Amesema kutokana na umuhimu huo mwelekeo wa Wizara yake ni kuzidi kuongeza maafisa ugani ikiwa ni pamoja na kuwapatia pikipiki na kuongeza bajeti.
“Tunanunua pikipiki kwa ajili maafisa ugani lengo likiwa ni kuwafikia wengi ikiwa ni pamoja na kufanya mafunzo,”amesema
JITIHADA KATIKA UMWAGILIAJI
Amesema Serikali itaendelea kuongeza jitihada katika umwagiliaji ikiwa ni pamoja na kufungua Skimu za umwagiliaji ambapo amedai wameongeza bajeti lengo likiwa ni kuwafikia watu wengi.
MASOKO
Waziri Mkenda amesema Wizara imekuwa ikitafuta masoko mbalimbali kwa ajili ya wakulima ambapo amedai kwa sasa wanataka kuvitumia vyama vya ushirika ili kuweza kuuza nje ya Nchi
“Tunaongeza jitihada katika masoko sasa hivi tuna kituo Juba South Sudan na tumeanza kuuza unga Kenya na tunataka kuuza katika maeneo mengine,”amesema.