Home Mchanganyiko ETDCO YATEKELEZA MIRADI 89 YA UMEME KWA SH. BILIONI 300

ETDCO YATEKELEZA MIRADI 89 YA UMEME KWA SH. BILIONI 300

0

Kaimu Meneja Mkuu wa Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji Umeme (ETDCO), Mhandisi Maclean Mbonile akielezea mafanikio ya kampuni yao katika miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara. Kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Nishati, Doreen Makaya.

*****************************

Na Mwandishi Wetu

KATIKA kipindi cha miaka mitano, Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji wa Umeme (ETDCO), imefanikiwa kutekeleza miradi 89, iliyogharimu shilingi bilioni 307.5.

Aidha kampuni hiyo tanzu ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), imepata faida ya shilingi bilioni 9.6 katika kipindi cha miaka mitano ya uwepo wake.

Hayo yote yamesemwa jijini Dar es Salaam leo na Kaimu Meneja Mkuu wa ETDCO, Mhandisi Maclean Mbonile wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya mafanikio waliyoyapata katika kipindi cha miaka 60 ya uhuru wa Tanzania Bara.

Mhandisi Mbonile alisema hadi kufikia mwaka 2017 wamefanikiwa kutekeleza miradi 74 ambayo imegharimu shilingi bilioni 156.03 ambayo ni ujenzi wa njia ya kusafirishia umeme wenye uwezo wa kilovoti 132 kutoka Mtwara hadi Lindi.

“Huu ulikuwa mradi mkubwa wa kwanza kutekelezwa na kampuni tangu kuanzishwa kwake, ulihusisha ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme yenye umbali wa kilomita 80 kutoka kituo cha umeme Mtwara hadi kwenye kituo cha umeme cha Mahumbika Lindi.

“Ukamlishwaji wa mrdai huu uliwezesha mji wa Lindi kuanza kutumia umeme unaozalishwa na mitambo inayotumia gesi iliyopo Mtwara badala ya matumizi ya umeme wa jenereta, mradi huu una thamani ya shilingi bilioni 11.4,” amesema Mbonile.

Alitaja mradi mwingine kuwa  ni ujenzi wa njia ya kusambaza umeme kutoka Morogoro hadi Mradi wa Uzalishaji Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) wenye uwezo wa umeme wa kilovoti 33 na urefu wa kilomita 54 ambao uliingizia ETDCO shilingi bilioni 5.8

Mbonile alisema pia kwa miaka mitano wamefanikiwa kutekeleza mradi wa ujenzi wa njia ya kupeleka umeme wenye uwezo wa kilovoti 33 kutoka Mahumbika hadi Ruangwa.

“Ujenzi huu wa njia ya umeme ya kilomita 120 ya njia pacha umekamilika mwaka 2018 na umegharimu shilingi bilioni 8.7, pia tumetekeleza mradi wa njia ya umeme kilovoti 33 kutoka Nanyumbu hadi Tunduru kwa thamani ya shilingi bilioni 1.5,” alisema Mbonile.  

Alisema pia wamefanikiwa kujenga njia ya umeme yenye uwezo wa kilovoti 33 kutoka Gongo la Mboto hadi JNHPP kwa lengo la kuimarisha upatikanaji wa umeme kwa mkandarasi wa mradi ambapo ujenzi ulianza mwaka 2019 na kukamilika Februari mwaka huu kwa thamani ya shilingi bilioni 17.

“Ujenzi wa njia ya kupeleka umeme wa kilovoti 33 wenye urefu wa kilomita 105, kutoka Geita hadi Mgodi wa Serikali wa STAMIGOLD wilaya ya Biharamulo, umegharimu shilingi bilioni 6.4 umekamilika Juni 2021,” alisema.

Mhandisi Mbonile alitaja mradi mwingine ni wa kupeleka umeme wa kilovoti 33, kwenye mjji wa Serikali Mtumba ambapo ni umbali wa kilomita 51, umegharimu  shilingi bilioni 3.4.

“Mbali na miradi iliyokamilika tunayo miradi 15 inayoendelea kutekelezwa, ambapo kwa pamoja itahusisha kupeleka umeme kwenye vijiji 194 na kugharimu takribani shilingi bilioni 64.5 ambayo itakamilika mwisho mwa 2022,” alisema.

.

“Pia tunatekeleza ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya uwezo wa kilovoti 132 kutoka Tabora kwenda Katavi na Tabora kwenda Kigoma, ambapo jumla ni kilomita 776, thamani ya miradi hii ni shilingi bilioni 15.9, itawezesha kufikisha umeme wa gridi ya taifa kwenye mkoa wa Katavi na Kigoma,” amesema.

Mbonile alitaja matarajio yao ni kuongeza uwezo kwenye ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya usafirishaji umeme mkubwa hadi kufikia zaidi ya kilovoti 400, kutoka huduma ya ushauri wa kitaalam, uwekaji umeme kwenye majengo na kufanya kazi nje ya Tanzania.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Nishati, Doreen Makaya alisema ETDCO, imekuwa mtekelezaji mkubwa wa lengo la Serikali kufikisha umeme kila kona ya nchi hivyo wataendelea kusapoti.

“Meneja ameelezea mafanikio ambayo wamepata, hili kwetu ni jambo jema kwani ndio lengo letu kuu kuhakikisha vijiji vyote 12,000 nchini vinapata huduma ya umeme, hivyo ETDCO akishirikiana na wazabuni wengine Tanzania itan’gaa,” alisema.