Na Joseph Lyimo, Babati
MRADI wa elimu ya haki ya afya ya uzazi kwa wanawake na wasichana kwenye wilaya ya Babati Mkoani Manyara, umefanikiwa baada ya hamasa ya kutolewa kwa taarifa za matukio ya ukatili kufikia asilimia 40.
Ofisa ustawi wa jamii wa halmashauri ya wilaya ya Babati, Mathias Focus amesema mwitikio wa kutolewa kwa taarifa za vitendo vya ukatili wa kijinsia ni mkubwa kuliko awali.
Focus amesema watu wengi wanajitokeza na kufika polisi, ofisi za ustawi wa jamii na maendeleo ya jamii kwa ajili ya kuripoti hivyo ni hatua kubwa kwa serikali na wadau katika kutekeleza miradi ya elimu kwa umma.
Mradi huo umetekelezwa na klabu ya waandishi wa habari wa mkoa wa Manyara (MNRPC) kwa ufadhili wa shirika la Women Fund Tanzania Trust (WFT).
Focus amesema miongoni mwa mafanikio hayo ni baada ya wanawake na wasichana wa kata ya Riroda kupewa elimu na MNRPC Oktoba mosi mwaka huu, amepokea malalamiko tisa kwa wanawake hao.
“Kwa mwezi napokea simu tatu hadi nne kwa wanawake waliopokea mafunzo kuwa wanahitaji kupata haki zao ikiwemo kutekelezwa kwa wanawake wenye watoto wao,” amesema Focus.
Amesema pia kuna malalamiko ya mjane aliyofikishiwa na kumwagiza aanze kwa ofisa mtendaji wa kijiji cha Riroda ambaye ana uhakika tatizo lake litapatiwa ufumbuzi mara moja.
Msichana mkazi wa Riroda, Elizabeth Matle amesema kupitia elimu hiyo amekuwa anawajengea uwezo wasichana wengine ambao hawakupata mafunzo hayo ili watambue haki zao.
“Kuna mwanamke alitelekezwa na mwanaume aliyezaa naye mtoto wake mwenye umri wa miaka miwili nikamwambia aende ofisi za ustawi wa jamii na sasa amepata haki yake kwani mwanaume anatoa matumizi ya mtoto,” amesema Matle.
Amesema hata hivyo anakabiliwa na wakati mgumu kwani baadhi ya watu wanamuona kuwa ni mtetezi wa wanawake na wasichana hivyo wanamchukia japokuwa yeye hajali hilo mradi anatenda haki.