Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Profesa Sifuni Mchome, akizungumza na Wakili wa Kujitegemea na Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili wa Tanganyika ( TLS Kanda ya Kagera Peter Mussa wakiwa nje ya Gereza la Wanawake Bukoba baada ya kuwatembelea na kufanya mazungumza na mahabusu na wafungwa wanawake na wanaume. Katibu Mkuu Mchome alimtaka Mwenyekiti wa TLS pamoja na mambo mengine kuzungumza na mawakili wenzie umuhimu wa kuzingatia maadili ya taaluma yao wakati wakitekeleza majukumu yao
…………………………………………………………………
Na Mwandishi Maalum, Bukoba
Mawakili wanaotoa msaada wa kisheria kwa watuhumiwa wa makosa mbalimbali yakiwamo ya jinai, wameshauriwa kutekeleza jukumu hilo kwa kuzingatia weledi wa taaluma zao na si vinginevyo.
Ushauri huo umetolewa mwishoni mwa wiki na Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, Profesa Sifuni Mchome, katika mazungumzo yake mafupi na Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili Tanganyika ( TLS) muda mfupi baada ya Ujumbe wa Makatibu Wakuu wakiongozwa na Profesa Mchome, kumaliza mazungumzo yao na mahabusu na wafungwa wanaume na wanawake waliopo katika Gereza la Bukoba.
Wakiwa ndani ya Gereza hilo upande wa Gereza la Wanawake, Makatibu wakuu hao walikumbana na kisa cha mahabusu mmoja ambaye amekaa ndani ya gereza hilo kwa zaidi ya miaka sita sasa akisubiri kukamilika kwa upepelezi wa tuhuma za mauaji anazokabiliwa nazo.
Mahabusu huyo aliwaeleza Makatibu Wakuu hao, kwamba licha ya yeye kuwa tayari kukili kosa lake na alikuwa tayari kufanya hivyo, lakini Wakili aliyekuwa anamsimamia alimkataza kukiri kosa lake kitendo ambacho kimemfanya aendele kusota Gerezani.
Ni kutokana na maelezo ya mahabusu huyo, ndipo Katibu Mkuu Profesa Mchome anapowataka mawakili kuzingatia weledi wa taaluma zao na kuacha kukikua maadili ya kazi zao.
“ Hapana naona kuna shida ya maadili hapa hakuna jambo jingine “ anasema Katibu Mkuu Mchome, na kuongeza “Bw. TLS, nikuombe hebu kaa na mawakili wako muliangalie hili, zungumzeni. Kama mtuhumiwa anataka mwenyewe kwa hiari yake kukili kosa lake mwacheni afanya hivyo, kwa sababu yeye ndiye anayejua ukweli wa nini alichokifanya, shaurini vizuri zingatieni maadili ya kazi zenu na taaluma zenu”. Akasisitiza Katibu Mkuu Mchome.
Katibu Mkuu Mchome, akaeleza pia kwamba kazi kubwa ya Mawakili na Wanasheria ni kutoa ushauri wa kisheria kwa weledi, maadili mema, kwa wakati na kufanya kazi kwa matokeo ili haki itendeke na na taifa liendelee kupiga hatua za maendeleo.
Katika hatua nyingine Katibu Mkuu Profesa Mchome amesema, atatuma timu ya Wanasheria Kutoka Wizara ya Katiba na Sheria ili kwenda kutoa msaada wa kisheria Mkoani Kagera.