Home Mchanganyiko KAMISHNA WA MAADILI AWAPIKA VIONGOZI WA MKOA NA TAASISI ZA SERIKALI MKOANI...

KAMISHNA WA MAADILI AWAPIKA VIONGOZI WA MKOA NA TAASISI ZA SERIKALI MKOANI MBEYA KUHUSU MAADILI YA VIONGOZI WA UMMA.

0

Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji Sivangilwa Mwangesi akitoa Mada kwa viongozi wa Mkoa wa Mbeya pamoja na Taasisi za serikali zilizopo Mkoani humo katika Semina iliyoandaliwa na Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Juma Homera iliyofanyika tarehe 23 Septemba, 2021 katika Ukumbi wa Benjamin Mkapa jijini Mbeya.

Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji Sivangilwa Mwangesi akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Juma Homera alipomtembelea ofisini kwake alipofanya ziara ya siku mbili mkoani Mbeya iliyompa fursa ya kuzungumza na viongozi wa Mkoa na Taasisi za Serikali zilizopo mkoani humo.

Mstahiki Meya wa Jiji la Mbeya Mhe. Issa Dor Mohamed Rahmat akichangia katika semina ya Maadili iliyoandaliwa na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Juma Homera kwa ajili ya Viongozi wa Mkoa pamoja na Taasisi za Serikali zilizopo mkoani humo iliyofanyika katika ukumbi wa Benjamin Mkapa tarehe 23 Septemba, 2021  ambapo Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji Sivangilwa Mwangesi alitoa Mada.

********************************

Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji Sivangilwa Mwangesi amehitimisha ziara yake ya siku mbili mkoani Mbeya kwa kukutana na kuwasilisha mada kuhusu Maadili kwa viongozi wote wa Mkoa pamoja na Taasisi za serikali  zilizopo mkoani humo.

Mkutano na viongozi hao ulifanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya wa Benjamin Mkapa na uliongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Juma Homera.

Akiwasilisha mada kwa viongozi hao Mhe. Mwangesi alianza kwa kuitaja na kufafanua misingi ya Maadili ambayo ni pamoja na kuwa muadilifu; muwajibikaji; muwazi; muaminifu na mkweli; na kuheshimu Sheria.

Mhe. Mwangesi aliendelea kutaja misingi mingine ya maadili ambayo ni kuzingatia haki na usawa; kuzuia mgongano wa maslahi; kutunza siri; kufanya maamuzi kwa zingatia ubora na ufanisi.

Kwa mujibu wa Mhe. Mwangesi kiongozi au Mtumishi wa umma anategemewa kuwa na Maadili haya ya msingi ambayo yatasaidia uzingatiaji wa masharti ya sheria kuhusu Maadili ya viongozi wa umma na sheria nyingine za nchi.

“Misingi hii ya Maadili ndiyo inayojenga tabia na mienendo ya kimaadili inayopaswa kuzingatiwa na viongozi wote wanaoshika nafasi za madaraka zilizotajwa katika Sheria.  Tabia na mienendo ya kimaadili ina mchango mkubwa katika kuepeusha uvunjaji wa Maadili kwa viongozi na watumishi wa umma nchini” alifafanua Mhe. Kamishna. 

Mhe. Mwangesi aliendelea kusema kuwa uzingatiaji wa viwango vya Maadili kwa viongozi wa umma unasaidia kuimarisha imani ya wananchi kuhusu uadilifu, haki na kutopendelea kwa Serikali. 

Katika kuweka mkazo wa suala hili Mhe. Mwangesi alimnukuu Jaji L’Heureux – Dube wa Mahakama ya Juu ya Kanada kuwa kutokana na imani kubwa na wajibu unaoambatana na wadhifa wa ofisi ya umma, ni muhimu kwa maafisa wa serikali kuwajibika chini ya kanuni za Maadili ambazo kwa raia wa kawaida zingeonekana kuwa ni kali zaidi alisema Mhe. Mwangesi.

Katika mada yake Mhe. Mwangesi aligusia pia baadhi ya mambo yanayochochea ukiukwaji wa Maadili ambayo ni pamoja na tamaa; kukosa uaminifu; kukosa uzalendo; ubinafsi na Mgongano wa Maslahi; upokeaji wa zawadi zisizoruhusiwa na sheria na matumizi mabaya ya madaraka.

 Akizungumza katika mkusanyiko huo wa viongozi wa Mkoa wa Mbeya, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe Juma Homera alisema kuwa Mkoa wa Mbeya kama zilivyo Taasisi nyingine za umma nchini unatekeleza Mkakati wa Udhibiti Rushwa Awamu ya Tatu wa mwaka 2017 hadi 2022.

Mhe. Homera aliendelea kusema kuwa utekelezaji wa Mkakati huo umelenga kukuza Uwajibikaji, Uwazi na Uadilifu katika matumizi ya rasilimali za umma kwa lengo la kuimarisha utoaji wa Huduma na ustawi wa wananchi.

Kwa mujibu wa Mhe. Homera, kupitia mafunzo haya utawaongezea weledi kwa Viongozi na Watendaji wa Mkoa wa Mbeya katika kutekeleza Mkakati wa kudhibiti Rushwa na Uadilifu katika Taasisi zote za umma zilizopo Mkoani Mbeya.