Home Mchanganyiko TBS YAWAPATIA ELIMU YA VIWANGO WAJASIRIAMALI KATIKA MAONESHO YA KITAIFA YA AU...

TBS YAWAPATIA ELIMU YA VIWANGO WAJASIRIAMALI KATIKA MAONESHO YA KITAIFA YA AU YA SIDO  KASULU MKOANI KIGOMA

0

Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma, Bw. Rashid K. Mchatta (wa kwanza kushoto) akizungumza na maafisa wa TBS ili kujua mwamko wa wajasiriamali kupata alama ya ubora mkoani Kigoma wakati alipotembelea maonesho ya kitaifa ya SIDO yanayoendelea wilayani Kasulu.

Kaimu Mkuu wa Kanda ya Magharibi (TBS), Rodney Alananga akitoa elimu kuhusiana na madhara ya vipodozi vilivyozuiwa vyenye viambata sumu kwa wananchi waliotembelea banda la TBS katika maonesho ya SIDO kitaifa wilayani Kasulu.

Wajasiriamali wadogo wakipatiwa elimu ya Viwango na kufanya utaratibu wa kusajili majengo yao ya chakula na vipodozi katika Maonesho ya Kitaifa ya Tatu ya SIDO wilayani Kasulu Mkoani Kigoma.

****************************

Na Mwandishi Wetu, Kigoma

WAJASIRIAMALI kutoka mikoa mbalimbali nchini waliohudhuria Maonesho ya Kitaifa ya Tatu ya SIDO wamepatiwa elimu kuhusu taratibu za kuthibitisha ubora wa bidhaa zao hususani kupitia mpango wa bure kwa wajasiriamali wadogo sambamba na utaratibu wa kusajili majengo yao ya chakula na vipodozi

Wajasiriamali hao wamenufaika na fursa hiyo kutoka kwa maofisa wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) katika maonesho hayo yaliyoanza Setemba 21, mwaka huu wilayani Kasulu mkoani Kigoma ambayo yalifunguliwa Septemba 22, mwaka huu na Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango.

Aidha, maofisa hao wa TBS walitoa huduma katika banda la kliniki ya biashara linalosimamiwa na TANTRADE lengo likiwa ni kumrahisishia mjasiriamali kupata huduma haraka bila kupoteza muda.

Akizungumza kwenye maonesho hayo Kaimu Mkuu wa Kanda ya Magharibi wa TBS, Rodney Alananga aliwashauri wajasiriamali kuzingatia kanuni za uzalishaji na uhifadhi bora na salama ili kuepuka kupoteza masoko na hasara ya kukutwa na bidhaa hafifu.

Pia aliwashauri kuwasiliana na ofisi ya TBS mara kwa mara pale wanapohitaji msaada wa kitaalamu.

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Uhusiàno na Masoko TBS, Gladness Kaseka alisema TBS hutoa elimu na mafunzo mbalimbali kupitia midahalo, semina, kampeni, maonesho, runinga, redio na mitandao ya kijamii.

“Huu ni mwanzo, kwani Shirika litahakikisha elimu ya viwango inamfikia kila mdau na katika ngazi ya chini kabisa. Leo tupo wilayani kasulu kupitia maonesho, lakini tumeshapita Kakonko, Kibondo na wilaya zingine zaidi ya 70 Tanzania kupitia kampeni za kuelimisha umma na semina za mafunzo.

Elimu na mafunzo tunayotoa ni bure, Serikali inagharamia kupitia TBS na tuna mpango wa kufika nzima,” alisema Kaseka.

Naye Afisa Masoko wa TBS, Deborah Haule aliwasisitiza wajasiriamali ambao bado bidhaa zao  hazijapatiwa nembo ya bora, kuchangamkia fursa ya bure kwa kutuma maombi ya kutumia alama ya ubora kupitia SIDO ili Serikali iwatambue kama wajasiriamali wadogo na kati na waweze kuhudumiwa bure kwa kuwa bidhaa nyingi wanazozalisha zinaangukia katika kiwango cha lazima, hivyo kulazimika kukidhi matakwa ya viwango kwa mujibu wa sheria.

Mwananchi, Abdallah Shaban aliipongeza juhudi zinazofanywa na TBS kuhakikisha wanawasaidia wadau wa sekta mbalimbali hususani wajasiriamali kuzingatia viwango ili kuweza kupata masoko ndani na nje ya nchi na kuwa na ushindani huru sokoni.

Hata hivyo aliitaka TBS kuhakikisha wnafanya kaguzi za mara kwa mara sokoni hasa maeneo ya vijijini ili kumlinda mlaji dhidi ya bidhaa hafifu na zile zilizokwisha muda wa matumizi au zisizotakiwa kabisa masokoni.

Kwa upande wa wajasiriamali wameiomba Serikali kurahisisha upatikanaji wa vifungashio ili waweze kuondokana na changamoto hiyo.

TBS ni mdau muhimu katika maonesho hayo hasa ukizingatia yanahusisha uoneshaji wa bidhaa mbalimbali za wajasiriamali wadogo kutoka mikoa yote ya Tanzania.

Kwa mwaka huu maonesho hayo yamehudhuriwa na wajasiriamali takribani 700 wakiwa na bidhaa kama vile unga, maji,juisi, asali, karanga, vipodozi mafuta ya kula, sabuni, korosho, mvinyo, mchele, samani, vitenge na mashine mbalimbali.