Na Mathias Canal, Wizara ya
Kilimo-Dar es salaam
Waziri
wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda (Mb) leo tarehe 2 Septemba 2021 amekutana na
kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkazi wa Kampuni ya Wilmar Tanzania Ndg Sachin
Suman katika ofisi za Wizara ya Kilimo zilizopo katika eneo la Tazara Jijini
Dar es salaam.
Waziri
Mkenda amekutana na Mkurugenzi huyo ambapo Kampuni yake inamiliki viwanda vikubwa 3 Mkoani Morogoro na
kuwahakikishia kuwa atatekeleza maagizo yaliyotolewa na serikali kwa viongozi
wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Uwekezaji na Mamlaka za Serikali za Mitaa
kuondoa urasimu unaokwamisha ujenzi wa viwanda nchini.
Katika
mkutano huo Waziri Mkenda amesema kuwa wamekubaliana kuhusu kuongeza uwekezaji
katika ukoboaji wa mpunga ili kuhakikisha kwamba unapatikana mchele mzuri ambao
utakuwa unauzwa zaidi kimataifa.
Amesema
kwa sasa kiwanda hicho kina uwezo wa kukoboa tani 100,000 kwa mwaka za mpunga jambo
ambalo amekitaka kiwanda hicho kuongeza uwezo wake kwani wana uwezo wa kufikia
mpaka tani 300,000 kwa mwaka kwa kuanzia.
Waziri
Mkenda ameeleza kuwa kwa kauli moja mkutano huo umekubaliana kuunda timu ya
wataalamu kutoka serikalini pamoja na kampuni hiyo ili ndani ya siku 30 itatakiwa
kuangalia maeneo mazuri ya kulima mpunga na kutoa mapendekezo ya namna kilimo
hicho kitakavyofanyika ili kuongeza tija na uzalishaji.
Amesema
kuwa kiwanda cha kukoboa mpunga (Murzar Wilmar Rice Mills Ltd) kilichojengwa
kwa gharama ya shilingi Bilioni 48 na ambacho kina uwezo wa kukoboa tani 288 za
mpunga kwa siku na kisha kufungasha mchele katika ujazo na madaraja mbalimbali
kitatoa fursa kwa wakulima kujihakikishia soko la uhakika wa mpunga.
Kiwanda
hicho kimeajiri wafanyakazi 75 na kinanunua mpunga kutoka kwa wakulima
takribani 5,000 kutoka Mikoa ya Morogoro, Mbeya, Shinyanga na Tabora ambapo
katika mwaka 2020 kimenunua tani 65,000 zenye thamani ya shilingi Bilioni 45.
Waziri
Mkenda amesema kuwa miongoni mwa makubaliano yaliyofikiwa katika mkutano huo ni
pamoja na kuwa na mashamba darasa kwa ajili ya wakulima na kuwa na maeneo ya
kukusanyia mazao ya kutoka kwa wakulima kwa ajili ya kupeleka viwandani.
Waziri
Mkenda amesema kuwa serikali italifanyia kazi kwa haraka ombi lao la kupatiwa
kibali na serikali kuzalisha umeme utakaotumika katika shughuli za kiwanda na mwingine
utakaosalia wataliuzia Shirika la Umeme (TANESCO).
Kuhusu
uzalishaji wa mazao ya mafuta ikiwemo alizeti na Soya kwa ajili ya kuzalisha
mafuta mengi ya kula, Waziri Mkenda amesema kuwa kampuni hiyo ipo tayari
kununua mazao hayo na kuyachakata, hivyo amewahakikishia kuwa serikali ina mkakati
madhubuti wa kuhakikisha uzalishaji wa alizeti unaongezeka kwa kiasi kikubwa
ikiwemo uzalishaji wa michikichi.
Mhe
Prof. Mkenda ameipongeza kampuni ya Murzar Wilmar Rice Mills Ltd kwa kuwekeza
katika kiwanda hicho kikubwa kuliko vyote hapa nchini kwa kukoboa mpunga.