Katibu Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa,Kenani Kihongosi akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 24,2021 Jijini Dodoma 

………………………………………………

Na.Alex Sonna,Dodoma

Katibu wa Umoja  wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa,Kenani Kihongosi amewatoa hofu wananchi kwa kuwataka  wazidi kuiamini Serikali yao na kuendelea kulipa kodi kwani kila senti inaenda kugusa maisha yao.

Hayo yamesemwa leo Agosti 24,2021 jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari Kihongosi amesema kuwa wiki iliyopita Waziri wa Fedha na Mipango,Dkt.Mwigulu Nchemba amesema takribani shilingi bilioni 48 zimekusanywa na kugawanjwa katika mambo mbalimbali ikiwemo ujenzi wa vituo 150 vya afya.

“Unapoenda  kujenga madarasa unamfanya mtoto   wa masikini aweze kusoma.Tunaipongeza Serikali kwani  fedha hizo zitaenda kurekebisha barabara na kila Jimbo liliishapewa zaidi ya shilingi milioni 500.Uchumi utaenda kuimarika katika maeneo ya vijijini na pato litaongezeka,”amesema

Hivyo,Kihongosi amewatoa hofu watanzania wazidi kuimani Serikali na kuendelea kulipa kodi kwani kila fedha inaenda kugusa maisha ya watanzania.

Hata hivyo,Kihongosi  ameiomba Serikali fedha hizo ziende zikafanye kazi iliyokusudiwa ili walengwa wazidi kuwa na maendeleo

“Tunaiomba Serikali fedha hizi ziende katika  kazi ile ambayo imekusudiwa wale walengwa husika waende wakagushwe na mambo haya yaweze kwenda vizuri,”amesema.

Aidha Kihongosi amewataka vijana kuendelea kuchapa kazi,kulipa kodi  na kuilinda kwa nguvu zote amani iliyopo ikiwa ni pamoja na kuheshimu Mamlaka.

“Uchumi imara utajengwa na vijana jambo lolote litasimamiwa na vijana wajibu wetu ni kuitii na kuheshimu mamlaka tukisoma historia wazee wetu walifanya kazi kubwa ya kujenga uchumi wetu,sisi wajibu wetu ni kuendeleza mema ili kizazi kinachokuja kitupongeze.

“Nchi hii ilikombolewa na vijana na itasimamiwa na vijana hivyo lazima vijana tulipe kodi kwani wahusika wakuu ni sisi.Niseme sisi kama vijana tutazidi kusimama  imara na tutazidi kuhakikisha tunailinda heshima ya Nchi yetu viongozi wetu wote kwa sababu tunaamini vijana ndio watu pekee wanaoweza kusema na serikali itakalitekeleza,”amesema

Kuhusiana na wale wanaoitukana Serikali katika mitandao,Kihongosi amesema : “Nitoe wito nidhamu ni mali na nidamu ni uadilifu,kijana utapimwa unapokosa nidhamu kwa mzazi wako na kiongozi wako maana yake  huna tofauti na msaliti lazima tuwe wazalendo tushirikiane na viongozi wetu.”

Pia amesema kuwa  hivi karibuni UVCCM itakuja na Programu ya kuandaa makongamano ya fursa pamoja na dira ya jinsi gani ya kutumia vipaji ili kuondokana na changamoto ya ajira.

Aidha amesema kuwa ziara anazofanya  Rais Samia Katika nchi mbalimbali zitasaidia kuondosha migogoro,kujenga urafiki kati ya nchi na nchi kudumisha amani na kufungua fursa mbalimbali.

“Fursa nyingi za kiuchumi,amani na ushirikiano tulionao na nchi nyingine  vinatokana na mahusiano mazuri yaliyopo ,kupitia ziara anazofanya Mama Samia itasaidia kuondoa migogoro isiyo ya lazima,”amesema Kihongosi