Home Mchanganyiko MAADHIMISHO YA KUMBUKIZI YA VITA VYA MAJIMAJI YA ZINDULIWA RASMI KILWA

MAADHIMISHO YA KUMBUKIZI YA VITA VYA MAJIMAJI YA ZINDULIWA RASMI KILWA

0

Mkuu wa Wilaya ya Kilwa Mhe, Zainabu Rashidi Kawawa, akihutubia wananchi wa Nandete
Kilwa, kwenye uzinduzi wa maadhimisho ya kumbukizi ya Vita vya Majimaji.

Mkuu wa Wilaya ya Kilwa Mhe, Zainabu Rashidi Kawawa, akiongoza wananchi mbalimbali
kutembelea Mapango ya Nang’oma, Tarafa ya Kipatimu Kilwa. Mapango hayo yalitumika
katika vita vya Majimaji. Maji yanayoonekana ndipo yalipochotwa maji yaliyotumika kama
dawa kwenye vita hivyo.

Wananchi mbalimbali wakiwa mbale ya mnara wa Mashujaa wa Vita vya Majimaji, Nandete Kilwa, kwenye Uzinduzi wa maadhimisho ya Kumbukizi ya Vita ya Majimaji  dhidi ya Wakoloni Kikundi cha Ngoma ya Kimatumbi wakicheza ngoma kwenye kwenye Uzinduzi wa maadhimisho ya Kumbukizi ya Vita ya Majimaji  dhidi ya Wakoloni vilivyo anzia Nandete .

Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Dkt Noel Lwoga pamoja na wananchi mbalimbali
wakiwa kwenye mapango ya Nang’oma, Tarafa ya Kipatimu Kilwa. Mapango hayo yalitumika
katika vita vya Majimaji dhidi ya Wakoloni.

***********************

Na Sixmund J. Begashe

Madhimisho ya Kumbukizi ya Vita vya Majimaji yamezinduliwa rasmi kijiji cha Nandete Wilayani Kilwa katika Mkoa wa Lindi na kuhudhuriwa na wakazi wa wilaya hiyo na maeneo ya jirani pamoja na Taasisi za Serikali zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii.

Akizungumza na wananchi katika maadhimisho hayo, Mkuu wa Wilaya ya Kilwa Mhe, Zainabu Rashidi Kawawa, ambaye alikuwa Mgeni Rasmi wa shughuli hiyo amesema Serikali itaendelea kuboresha miundombinu na kuvutia wawekezaji ili mazingira yawe rafiki kwa watalii watakao tembelea vivutio vilivyomo Nandete.

 Mhe Kawawa amesema Wilaya ya Kilwa ina utajiri mkubwa wa urithi wa kihistori hasa eneo zima la Nandete ambako ndipo vita vya Majimaji vilianzia na kushika kasi sehemu mbali mbali za Kusini mwa Tanzania na hatimaye kumalizikia Songea, Mkoani Ruvuma.

Amesema yeye kama Mtendaji Mkuu wa Serikali Wilayani Kilwa atahakikisha maeneo hayo yanatambuliwa kisheria na kutangazwa kwa nguvu zote.

 Mhe Kawawa alizipongeza taasisi zote za Serikali hasa Makumbusho ya Taifa kwa kushiriki vyema katika kufanikisha maadhimisho hayo kwa kutoa wataalam walioshirikiana na wale wa Halmashauri ya Kilwa pamoja na kuhakikisha uzinduzi huo unatangazwa kwa njia mbali.

 Naye Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Dkt. Noel Lwoga licha ya kuahidi kuwa taasisi yake itaendeleza ushirikiano na Halmashauri ya Kilwa, amesema uzinduzi huo ni hatua muhimu ya kuelekea kwenye maadhimisho makubwa yatakayofanyika Songea Mkoani Ruvuma mwezi Februari mwakani.

 “Sisi kama Makumbusho ya Taifa tunahusika katika kutoa ushauri, kuhifadhi na kuendeleza urithi wa asili na utamaduni na kutafiti masuala haya ya kihistoria, hivyo tupo tayari kushirikiana nanyi na wadau wengine, kwa jinsi mtakavyoona inafaa, kufanya utafiti na kuanzisha kituo cha kimakumbusho hapa Nandete” Alisema Dkt Lwoga

 Katibu wa Baraza la Wazee Kijiji cha Kipatimu Tarafa ya Nandete, Mzee Abdalah Butoli amesema eneo la mapango yaliyotumika katika vita vya majimaji ni sehemu muhimu ya kuikumbusha jamii juu ya uzalendo na mshkamano wa kitaifa, huku Mzee Mwangosongo akiwashauri vijana kujifunza historia nchini yao badala ya kukaa kwenye vijiwe na kubadilishana tabaduni za kigeni.

 Uzinduzi wa Madhimisho hayo uliambatana na kutembelea maeneo mnara wa kumbukumbu ya mashujaa wa vita pamoja na mapango yaliyo tumika katika vita hivyo vilivyo piganwa kwa muda mrefu zaidi ya vita vingine Afrika dhidi ya Wakoloni.