Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji wa Rufani Sivangilwa Mwangesi akitoa mada katika kikao cha Viongozi wa Umma wa Mkoa wa Tabora kilichofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo mwishoni mwa wiki.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe. Balozi Dkt. Batilda Buriani akitoa neno la ufunguzi katika kikao cha Viongozi wa Umma wa Mkoa wa Tabora kilichofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo mwishoni mwa wiki. Kushoto kwake ni Kamishna wa Madili Mhe. Jaji Sivangilwa Mwangesi.
Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji Sivangilwa Mwangesi akijadiliana jambo na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe. Batilda Buriani alipomtembelea ofisini kwake (Tabora) mwishoni mwa wiki.
Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji Sivangilwa Mwangesi akitoa mada katika kipindi cha Mseto cha Charles George (CG) FM redio kilichopo Mkoani Tabora mwishoni mwa wiki.
…………………………………………………………
Viongozi wa Umma nchini wameaswa kujali maslahi ya Umma ambayo ndiyo msingi mkuu wa Serikali yeyote duniani.
Hayo yalisemwa na Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji wa Rufani Sivangilwa Mwangesi alipokua akitoa mada katika kikao cha Viongozi wa umma wa Mkoa wa Tabora kilichofanyika mwishoni mwa wiki mkoani humo.
Mhe. Mwangesi alisema kuwa kiongozi yeyote wa Umma ni kioo cha jamii husika hivyo, hana budi kujali maslahi ya Umma ikiwa ni pamoja na kuwa mzalendo kwa nchi yake, kufanya kazi kwa uaminifu, huruma, umakini, kijizuia na tamaa na kuzingatia viwango vya juu vya maadili pamoja na kuzingatia Sheria taratibu na miongozo mbalimbali.
“Viongozi wanapaswa kuwa na mienendo mizuri isiyotiliwa shaka ili waweze kuaminika katika jamii inayowazunguka,” alisema na kuongeza kuwa, kiongozi yeyote anapokua muadilifu kwa watu anaowaongoza bila shaka atapata heshima anayostahili katika jamii na nchi kwa ujumla
Mhe. Mwangesi alisisitiza kuwa “kiongozi ambaye ni muadilifu hufanya mambo mazuri hata pale ambapo hajaambiwa afanye ama pale ambapo hakuna anayemuona lakini kwa yule ambaye si muadilifu anaweza kufanya mambo mengi kwa kutumia nguvu na asifanikiwe hivyo nawaasa viongozi kuwa waadilifu jambo ambalo litarahisisha utendaji kazi wenu.”
Katika hatua nyingine Jaji Mwangesi aliwakumbusha viongozi wa umma baadhi ya misingi ya maadili ikiwa ni pamoja na kufanya maamuzi kwa kufuata sheria, kanuni, miongozo kwa manufaa ya umma, kujiepusha na migongano ya maslahi, kuepuka mienendo inayo aibisha utumishi wa Umma, na kuzingatia mipaka ya matumizi ya madaraka.
Awali akifungua kikao hicho Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe. Balozi Dkt. Batilda Buriani alisema kuwa Viongozi wote wa umma wanapaswa kuwa waadilifu na kuepuka mgongano wa maslahi
Mhe. Batilda alisema kuwa amefurahishwa na ziara ya Kamishna wa Maadili mkoani humo kwani ni wazi kuwa ujio wake unawakumbusha viongozi wa umma kukumbuka na kujitathmini kupitia kiapo cha Ahadi ya Uadilifu walichoapa mara tu walipoapishwa kuwa Viongozi.
Kikao hicho cha Kamishna wa Maadili na Viongozi wa Umma ni sehemu ya mikakati ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kutoa elimu ya Maadili kwa wadau wake.